The House of Favourite Newspapers

Yanga yaipiga Alliance bao 1-0, Amissi Tambwe Noma!

STRAIKA Amissi Tambwe wa Yanga ambaye rekodi yake ya mabao 21 ya msimu wa 2015/16 haijafutwa kwenye Ligi Kuu Bara jana alifanya yake. Guu lake moja tu la dakika ya 74 lilitosha kuwapa Yanga pointi tatu huku wakifikisha pointi 64 ambazo ni tofauti ya pointi 16 dhidi ya Simba wenye 48.

 

Tambwe ambae ni mchezaji pekee kwenye Ligi Kuu Bara anayeendesha gari kali zaidi aina ya V8,pasi ya bao lake ilitoka kwa Heritier Makambo. Mchezo huo ulikuwa na ushindani wa aina yake huku Alliance wakionekana kujiamini na kushambulia ingawa mabeki wao walifanya fyongo kwa kumkwatua Makambo dakika ya sita ya mchezo na kuwapa Yanga penati. Hatahivyo, Makambo aliipiga hovyo penati hiyo akakosa na kuwarudisha mchezoni Alliance ambao dakika ya 63 walifunga bao mwamuzi akasema wameotea.

Alliance ambao walionekana kuimarik a jana, walikosa nafasi nyingi huku wachambuzi wakidai kwamba uwepo wa Klaus Kindoki langoni mwa Yanga ulikuwa ukiwapa munkari wa kushambulia kusaka ushindi na
matumaini ya kupata bao.

 

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera jana aliwapumzisha kipa Ramadhani Kabwili na nahodha Ibrahim Ajibu makusudi huku akisisitiza kwamba alifanya hivyo kwa Ajibu kwavile kiwango chake mazoezini hakikuwa kizuri. Zahera aliwatoa Deus Kaseke/Said Makapu, Mrisho Ngassa/Tambwe na Haruna Moshi/Banka.

 

Katika mchezo wa jana, Yanga ilipiga mashuti manne ya maana langoni sawa na Alliance, Kona za Alliance zilikuwa sita na Yanga tatu. Faulo zilionekana kuwa nyingi zaidi kwa Alliance ambao walicheza 23 huku wenzao wakifanya 20, Yanga hawakuotea kabisa katika mchezo huo. Kadi za njano Alliance walionyeshwa mbili na Yanga moja katika mchezo huo ambao Yanga walizidiwa umiliki wa mpira kwa asilimia 57 kwa 43. Mchezo wa jana ulikuwa ni wa sita kwa Yanga kucheza ndani ya Kirumba kwenye Ligi Kuu tangu msimu wa 2011.

Comments are closed.