The House of Favourite Newspapers

Baraza la Maaskofu (TEC) Latoa Wito wa Kuheshimiana

0

BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania (TEC), limewataka Watanzania kuacha siasa za upendeleo na ubinafsi, kwa kuwa zinasababisha mfarakano katika kijamii.

 

 

Wito huo umetolewa na TEC kupitia ujumbe wake wa Kwaresma uliotolewa hivi karibuni, ukiwa na kichwa cha habari “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu…” (Zab 95:7-8).

 

 

Leo Jumatano, tarehe 17 Februari 2021, Wakristo wengi duniani wameanza ibada ya Kwaresma. Kwenye ujumbe huo wenye kurasa 29, umehusisha maaskofu 33 akiwemo Rais wa TEC, Gervas Nyaisonga, umeelezea mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiroho ukisema, kwa sasa dunia imeshuhudia manung’uniko na malalamiko kutoka kwa umma.

 

 

Malalamiko hayo ni juu ya baadhi ya viongozi wanaotumia mamlaka zao kufanya mambo kwa ajili yao na wanaowazunguka ama kikundi fulani, jambo linalokuza mashaka na kuondoa uaminifu.

 

 

“Licha ya hayo yote mema ambayo wenye mamlaka hususani ya kisiasa wamekabidhiwa, nyakati zetu hizi dunia, imeshuhudia manung’uniko na malalamiko kutoka kwa umma kwamba baadhi ya viongozi, wanatumia dhamana hiyo kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe au kwa ajili ya manufaa ya kikundi fulani.”

 

 

“Siasa za namna hiyo, husababisha unyanyasaji wa baadhi ya watu au kikundi cha watu na hivyo kuondoa hali ya kuaminiana,” limeeleza baraza hilo la juu la Kanisa Katoliki.

 

 

Ujumbe huo umeeleza wazi kwamba, miongoni mwa mipasuko mikubwa ya kisiasa inayotokea katika jamii, huchagizwa na kutokana na kikundi cha watu fulani kujiona ni wa daraja la juu na bora kuliko kingine.

 

 

Na kwamba, kikundi hicho wakati mwingine kujiona kiko juu ya Katiba na Sheria mbalimbali za nchi na hivyo kuzivunja pasi na kujali.

 

 

“Matokeo ya haya yote ni kufarakana kijamii, lawama zisizoisha na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa jamii husika,” umeeleza waraka huo.

 

 

Ujumbe huokutoka Kitabu cha Zaburi 95:7-8 ‘Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu,’ umewakumbusha Watanzania kurudi kwenye misingi ya Mungu ili kuleta uongozi bora na siasa safi.

 

 

“Kati ya maeneo muhimu sana ya kipimo cha uongozi bora na siasa safi, ni namna kiongozi anavyoishi uadilifu wake wa uongozi tukitambua kwamba “Hakuna mamlaka (halali) isiyotoka kwa Mungu”(Rum 13:1). Kutokana na hilo, uongozi, madaraka au mamlaka yoyote ile inapaswa kuwa ni dhamana kutoka kwa Mungu.

 

 

“Dhamana hii anapewa kiongozi kama mwakilishi wa Mungu katika uongozi tukitambua Mungu ndiye kiongozi na mtawala pekee. Dhamana hii inapaswa kumkumbusha kiongozi kwamba, mamlaka aliyopewa si kwa ajili yake bali ni kwa ajili ya wote aliokabidhiwa,” umekumbusha waraka huo.

 

 

TEC limewataka Watanzania kusikia sauti ya Mungu kwa kufanya toba na kuilainisha mioyo yao, katika kuhakikisha haki inatendeka katika jamii.

 

 

“Ujumbe wa Kwaresima unatutaka kama jamii “tusikie sauti yake, tusifanye migumu mioyo yetu. Tutaisikia sauti ya Mungu kwa kuhakikisha kwamba haki inatendeka katika jamii.

 

 

“… na hasa haki za kikatiba za kujiendesha kisiasa zikiwemo kuheshimu uhuru wa mawazo mbadala, kama sehemu ya kudumisha demokrasia na hasa katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ,” umeeleza ujumbe huo.

Leave A Reply