The House of Favourite Newspapers

Basi la Yanga Laharibika Moro, Mechi Leo Singida

0

MTANDAO wa Global Publishers umetinga gereji ya kampuni ya mabasi ya Al –Saed kujua maendeleo ya utengenezwaji wa basi la Klabu ya Yanga ambalo liliharibika ghafla mkoani hapa likiwa njiani kuelekea Singida ambapo leo jioni timu hiyo inakipiga na wenyeji wao, Singida United.

 

Baada ya kutinga kwenye gereji  hiyo kuu ya Al-Saed iliyopo maeneo ya Msamvu licha ya ulinzi mkali,   mwandishi wa mtandao huu ambaye anafahamika vizuri kwenye gereji hiyo,  alifunguliwa geti na kutinga ndani na moja kwa moja alikutana na mmiliki wa kampuni hiyo mzee Edha Al-Saed  maarufu kama Mzee Kipara.

Baada ya kuelezwa lengo la mwandishi huyo kutinga kwenye gereji hiyo mzee, Al-Saed alisema: “Shekidele kama unataka kupiga picha mabasi yangu piga picha hata mia ila kama unataka kupiga picha basi la yanga japo lipo kwenye gereji yangu sina mamlaka ya kukuruhusu; nenda kaongee na dereva wa basi hilo yule pale mwenye fulana ya SportPesa.”

 

Akizungumza na mtandao huu, dereva wa basi hilo alikataa basi hilo kupigwa picha sambamba na kugoma kutaja ugonjwa wa basi hilo licha ya kubwana kwa hoja kwamba timu hiyo ni ya wananchi na wananchi hao wanataka kujua kupitia waandishi wa habari ugonjwa wa basi lao na matengenezo yanaendeleaje na timu yao itafika vipi Singida.

 

Dereva huyo alijibu: “Kuharibika kwa gari ni jambo la kawaida na hili basi halina ugonjwa mkubwa, timu imeshafika Singida na basi la kukodi, tumefanya hivyo kwa lengo la kuwakwepa maadui zetu kama unavyojua tumeshafungwa mechi mbili mfululizo maadui zetu wanatuandama sana hivyo timu kwenda Singida na basi lingine ni mmoja ya njia za kukwepa hujuma za wapinzani wetu.

 

“Kuhusu kupiga picha mimi sina mamlaka ya kukuruhusu labda uende kwa Hamad lslama akikuruhusu mimi sitakuwa na kikwazo,” alisema dereva huyo aliyegoma pia kutaja majina yake.

 

Wakati Mwandishi akitoka kwenye gereji hiyo alishuhudia kundi la mafundi wakiwa chini ya uvungu wa basi hilo huku Properer Shafti ya basi hilo ikiwa tayari imeshatolewa nje.

 

Mwandishi wa habari hizi alipiga gia bodaboda yake hadi mjini eneo la Juwata lilipo duka la Hamad lslam ambapo tajiri huyo mwanachama na mfadhili wa timu hiyo mkoani hapa naye aligoma basi lao kupigwa picha likiwa gereji.

 

“Kweli basi letu limeharibika liko gereji ya Al- Saed lakini hatutaki lipigwe picha; kama unataka picha za basi ingia kwenye mtandao,” alisema lslama na kuongeza:

 

” Labda ukaandike habari kwamba mabasi ya Yanga na Simba yamechakaa yana muda mrefu sana toka udhamini wa Kilimanjaro mpaka leo zaidi ya miaka kumi, nadhani habari hiyo itasaidi timu yetu kupata basi jipya,” alisema tajiri huyo ambaye kabla ya Yanga kwenda Singida aliwaandalia chakula cha jioni nyumbani kwake.

 

MAONI YA MWANDISHI

Kiukweli mabasi ya Simba na Yanga yamechoka, yana muda mrefu sana kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, mabasi hayo walikabidhiwa mwaka 2012 wakati wanaingia udhamini na kampuni ya bia ya Kilimanjaro.

 

Hivyo kwa usalama wa wachezaji wetu wa Yanga na Simba wanaosafiri na mabasi hayo ‘micharaka’ kila siku, iko haja wadhamini walipe kipaumbele suala la kununua mabasi mapya kwa usalama wa wachezaji wa timu hizo pendwa nchini.

Na Dustan Shekidele, Morogoro.

Leave A Reply