The House of Favourite Newspapers

Mkwasa: Awashusha Presha Yanga, Kuifunga Singida United leo

0

UNAWEZA ukawa umesahau kutokana na changamoto za Januari lakini Yanga haijashinda mechi yoyote ya Ligi tangu mwaka wa 2020 uanze. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa dhidi ya Prisons Desemba 24 walipokuwa wanawapa mashabiki wao zawadi ya Krismasi, Yanga ilishinda bao 1-0 likifungwa na Patrick Sibomana.

 

Lakini Kocha msaidizi wa timu hiyo, Charles Mkwasa amewashusha presha mashabiki na kuahidi ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya Singida United ambayo hali yao si nzuri kwenye msimamo wa msimu huu.

 

Yanga ilipoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 3-0 na kupoteza wa pili dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0, leo watakuwa wageni wa Singida United katika Uwanja wa Namfua mkoani Singida.

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkwasa alisema kuwa anafahamu maumivu waliyoyapata mashabiki wa timu hiyo, hata wao benchi la ufundi na wachezaji hawafurahishwi na matokeo waliyoyapata hivi karibuni hivyo wamejiandaa vizuri kupitia mchezo dhidi ya Singida kuhakikisha wanapata ushindi mnono.

 

“Hakuna mpenzi yeyote wa Yanga, benchi la ufundi, kiongozi na wachezaji wanaopendezwa na matokeo tuliyoyapata hivi karibuni, hivyo tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wetu wa  leo  dhidi ya Singida United.

 

“Malengo yetu ni kupata ushindi katika kila mchezo hakuna anayependa kufungwa, wote tunapata maumivu pindi tunapopata matokeo mabovu, mashabiki wasiwe na wasiwasi kwani wachezaji wote wapo fiti kwa ajili ya kupambana na kupata ushindi,” alisema kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.

 

Yanga kwenye msimamo wa ligi inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi 25 katika michezo 14 waliyocheza, huku Singida United ikishika nafasi ya pili kutoka mwisho ikiwa na pointi 10 pekee.

Marco Mzumbe, Dar es Salaam

Leave A Reply