ILIPOISHIA…
MPENZI msomaji kama ndiyo umeanza kufuatilia simulizi hii ya maisha ya staa wa Bongo Muvi, Wastara Juma bado hujachelewa.
Ni wiki ya pili tu Wastara anasimulia juu ya simulizi ya kusisimua ya maisha yake na wiki iliyopita alisimulia namna masaibu kwenye maisha yake yalivyoanza kumpata tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
Alisimulia wakati mama yake akiwa na ujauzito wake wa miezi sita tu wachawi walimtokea na kumtaka yeye aliyekuwemo tumboni.
Wastara akasimulia pia kuwa hakunyonya maziwa ya mama yake kama watoto wengine kutokana na mama yake kuugua sana baada tu ya kujifunga, akasimulia pia namna alivyougua sana Ugonjwa wa Kifadulo na kuishia kusimulia alivyopata ajali mbaya ya pikipiki ambayo ilimfanya kuwa mlemavu na kwa muda wa miaka miwili akawa anasota chini!
…SASA ENDELEA
“MAMA na ndugu zangu walifahamu kuwa ndiyo hivyo tena ningemaliza maisha yangu nikiwa nasota chini, ndiyo maana nilisimulia wiki iliyopita kuwa walinirudisha nyumbani na nikaendelea kupata tiba za kienyeji.
“Hata hivyo, zilinisaidia kwa kiasi kikubwa maana baada ya miaka miwili nikiwa nasota chini nilianza kusimama kama mtoto mdogo anayejifunza kutembea. Nilikuwa nikisimama na kudondoka na baadaye nikaanza kutembea kwa kushika ukuta lakini nikiuachia nadondoka chini.
“Hali hiyo nayo iliendelea kwa muda wa mwaka mmoja ndipo Mungu aliponisaidia nikaweza kufanikiwa kurudi kwenye hali yangu ya kawaida ya kutembea kabisa na hatimaye nikaanza kukimbia,” anasimulia Wastara.
Anaendelea kusimulia kuwa baada ya kupona mama yake alimsafirisha pamoja na kaka yake mpaka Mlandizi ambapo kulikuwa ni maskani ya bibi yake mzaa mama. Wastara anasimulia kuwa walielekea huko kwa ajili ya kushiriki Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani.
“Sasa katika siku ya kwanza ya mfungo asubuhi bibi alituambia na kaka yangu tusifunge na tuanze siku iliyofuata. Tulikubali na jioni yake alitutuma kufuata mabarafu ya kugandishia juisi kwenye mji wetu mwingine ambao ulikuwa juu kidogo ya pale bibi alipokuwa anaishi.
“Mbali na kututuma nakumbuka bibi alitupa fedha, ambayo kama sikosei ilikuwa ni kama shilingi kumi hivi ambapo mimi na kaka yangu tuligawana shilingi tano – tano . Tukiwa njiani nilimwambia kaka yangu fedha zetu zote tuz inunul ie mapochopo cho na tule.
“Akaniuliza kwa nini nikamwambia nilitaka tuzimalize kabisa maana njiani tungegongwa na gari na tusingeweza kupata muda wa kuzitumia tena. Kaka yangu alikataa akaniambia kama mimi ninanunua basi ninunue lakini yeye angenunua baadaye na tusingeweza kugongwa na gari,” anasimulia Wastara na kuendelea kuwa;
“Nilimsisitiza juu ya hilo lakini aliendelea kukataa, nikaamua kununua kwa upande wangu. Nakumbuka nilinunua maembe, machungwa, miwa na vitu vingine kibao nikajaza kwenye gauni langu la bwanga ambalo nilikuwa nimevaa. Kaka naye aliniomba tukawa tunatembea huku tunakula.
“Sasa ile tunaendelea kutembea kuna sehemu tulifika tukatakiwa kuvuka barabara. Tukiwa hapo kabla ya kuvuka kuna mwanaume naye alifika na alikuwa anaendesha baiskeli. Alipotaka kuvuka alisimama kuangalia huku na huko na sisi tukashika baiskeli ili kuvuka naye.
“Akaendelea kuongoza huku tumeshika kitako cha nyuma lakini alipofika katikati ya barabara alituacha na kuangalia pembeni yetu kuna kosta (basi dogo aina ya Toyota Coaster) lilikuwa linakuja kutokea Dar likafika na kutupitia PUUU, kaka yangu akarushwa upande mwingine na mimi nikarushwa mbele barabarani kwenye lami.
“Lile kosta likawa bado lina endelea kuondoka, likanikuta mbele na kuanza kuniburuza chini kiasi kwamba sehemu ya kichwani nikapasuka na likanichuna kabisa sehemu kubwa ya ngozi ya uso.
“Sasa kwa upande wa kaka yangu kule alikodondokea alivunjika miguu yote miwili, lakini hakuweza kugundua mara moja kwa hiyo hata alipodondoka aliinuka na kuanza kulikimbiza kosta huku akilia kutaka aonyeshwe mdogo wake alikuwa wapi lakini kabla hajafika popote alidondoka chini.
“Hata hivyo, kwa bahati nzuri pale karibu na tulipopatia ajali kulikuwa na duka la dada yetu kwa hiyo aliona namna tulivyogongwa akaja anakimbia huku analia, watu wakajaa na pia dereva wa kosta hawakukimbia zaidi walielekea kuripoti kwenye Kituo cha Polisi kuwa wamegonga watoto na mmoja ambaye ni mimi alikuwa amefariki.
“Mama naye alipewa taarifa hizohizo, mama yangu alilia mno kusikia nimefariki, ndugu pia waliumia sana kwa taarifa hiyo, ikabidi waje hospitali ambako tulisaidiwa na wasamaria wema kujua hali ya yule waliyeambiwa yupo hai!”
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.