The House of Favourite Newspapers

Bavicha Wamuomba JPM Aunde Tume Huru

0

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yanayotokea nchini.

Baraza hilo limesema kwamba Rais  John Magufuli anapaswa kuunda tume hizo huru za kiuchunguzi zikiwahusisha watu kutoka nje ya nchi ili kusiwepo na kigugumizi wala upendeleo katika kufanya kazi hiyo.

Mwenyekiti wa baraza hilo Patrobas Katambi amesema hayo  leo Septemba 9 kwamba tume hiyo ambayo itakuwa na kazi ya kuwachunguza watu wasiojulikana inapaswa kukihusisha chama chao kwa sababu  viongozi wao wengi wamekumbwa na  vitendo hivyo.

“Yamekuwa yakitokea mauaji, kutishiana silaha, utekaji na kujeruhi lakini vyombo vya dola vimekuwa vikisema wanaofanya hivyo ni watu wasiojulikana.  Jambo ambalo linaashiria  watu hao wanaizidi nguvu Serikali,” anasema Katambi.

“Ni muhimu kuchukua hatua hiyo kwani watu hao wasiofahamika wanaweza kumdhuru yeyote  hata Rais wa nchi au yeyote mwenye damu” anasema Katambi.

Anasema vijana wa Bavicha wapo tayari kushirikiana Polisi masaa 24 na siku 360 ili kuwabaini watu hao wasiofahamika ambao wamekuwa tishio kwa usalama wa nchi.

“Hakuna mtu aliyewahi kufanya uhalifu duniani kote na asifahamike ni hapa tu kwetu kila tukio tunaambiwa wahusika hawajafahamika. Bora hata itumike picha ya Setilite lakini mtuhumiwa apatikane nadhani hapa kinachokosekana ni utashi tu,” anasema.

Kuhusu suala ka kupigwa risasi kwa kada wa chama hicho Tundu Lissu Katambi anasema vyombo vya dola bado vinafanya kazi yake lakini wao wanaweza kufanya na kudadavua tu mazingira ya tukio hilo na kujua wahusika.

“Nimewahi kulala kwa Lissu pale Dodoma kipindi nina kesi katika mji ule, nyumba yake iko  jirani na nyumba ya Spika na katika eneo lile wanakaa mawaziri. Ni eneo ambalo linalindwa wakati wote lakini watu wasiojulikana wameweza kupita na kufanya uhalifu.

Anasema tayari baraza hilo lilikwishamwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro kuhusu tishio la usalama wa kiongozi huyo lakini hakujibu.

“Agosti 24 nilimuandikia barua IGP kuhusu hofu ya usalama wa kiongozi wetu kama ambavyo taratibu zinaruhusu kutoa taarifa hata kama hofu hiyo haipo juu yako lakini jana amesema kuwa hakuwa na taarifa rasmi za Lissu,” anasema na kuendelea

‘’Endapo Jeshi la Polisi linasita kuchukua hatua vijana hao watachukua jukumu la kuwashughulikia watu hao wasiojulikana kwa namna isiyojulikana ili mradi kulinda hali ya usalama wa nchi kama lilivyo jukumu la kila  Mtanzania’’ anasema

Anasema  utaratibu huo ukishindikana atajiuzulu kwa sababu  atakuwa ameshindwa kusimama kama kiongozi wa vijana.

“Natoa agizo kwa viongozi wote wa vijana  nchi nzima kuratibu na kuonyesha namna wanavyokerwa na vitendo hivi vya uvunjifu wa amani, zoezi hili lifanyike kwa namna isiyojulikana na siku isiyojulikana,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa baraza hilo Julias Mwita amesema Bavicha wamewahi kutoa taarifa kuwa nchi inavimba kutokana na matendo ya viongozi wa Serikali hasa wateule wa Rais lakini taarifa yao ilipuuzwa.

“Matendo ya viongozi hao yanachochea yanajenga chuki na uhasama miongoni mwa watu. Hata Lissu alitoa taarifa kuhusu usalama wake akapuuzwa lakini ungekuwa uchochezi angefuatiliwa,” anasema Mwita.

Anasema jeshi la polisi linapaswa kuwa sikivu na vijana wote wakakamavu na wenye uwezo wa kuhoji katika taifa hili wasikubaliane na mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Watanzania

Leave A Reply