The House of Favourite Newspapers

Beki Rasta Atembea na Mkataba wa Yanga

0

 

BEKI wa pembeni wa Yanga, rasta Jaffary Mohammed, amesema kuwa anasubiri kusaini mkataba mpya kuendelea kubakia kwenye klabu yake hiyo.

 

Rasta huyo ni kati ya wachezaji wanaomaliza mikataba yao ya kuendelea kukipiga Yanga mwishoni mwa msimu huu, wengine baadhi ni Deus Kaseke, Kelvin Yondani, Juma Abdul na Issa Mohammed ‘Banka’.

 

Beki huyo anayemudu kucheza nafasi ya kiungo, alijiunga na Yanga kwenye msimu wa 2018/2019 akitokea Majimaji ya mkoani Songea baada ya kushuka daraja.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Jaffar alisema kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea kati yake na mabosi wake na kama yakienda vizuri, basi haraka atapewa mkataba na kusaini.

 

Jaffar alisema kuwa kwa hivi sasa hafikirii kuihama klabu hiyo kutokana na malengo yake aliyojiwekea kabla ya kuondoka hapo, ikiwemo kuipa ubingwa wa ligi unaoshikiliwa na watani wao, Simba.

 

Aliongeza kuwa, anaendelea kujifua kivyake sasa hivi katika kujiweka fiti zaidi wakati huu wa janga hili la Virusi vya Corona ili asipoteze nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

 

“Mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu, yapo mazungumzo mazuri yanayoendelea kati yangu na viongozi wa Yanga ya kuhitaji kutaka kunibakisha.

 

“Kama mazungumzo hayo yatakwenda vizuri, basi nitasaini mkataba mwingine wa miaka miwili wa kuendelea kuichezea Yanga katika msimu mwingine,” alisema Jaffar.

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply