The House of Favourite Newspapers

Simulizi Wazee Waliohukumiwa Kunyongwa Inasikitisha!

NJOMBE: Simulizi ya wazee watatu, Yohana Chengula (71), Aloyce Mwalongo (80) na Raphael Mlyuka (75), wakazi mjini Njombe, Tanzania ambao ni miongoni mwa wazee watano waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, inasikisha, Ijumaa linaanza kuismulia.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la Ijumaa wiki iliyopita ambayo yataruka kuanzia leo kupitia Global TV Online, wazee hao wanasema kamwe hawataisahau Desemba 9, 2017, siku ambayo waliachiwa huru kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’.

 

Wafungwa hao walipata msamaha wa Rais Magufuli wakiwa wamesota gerezani kwa zaidi ya miaka 40. Walikuwa wakitumikia adhabu ya kunyongwa hadi kufa, lakini baadaye ilibadilika na kuwa kifungo cha maisha.

 

Wazee hao walitiwa hatiani kwa makosa ya mauaji mwezi Machi, 1978, makosa ambayo wenyewe wanasema yalikuwa ni ya kubambikiwa.

 

CHENGULA

Akizungumzia maisha mapya nje ya gereza, Chengula anasema; “Namshukuru sana Mungu kwa sasa nipo uraiani, nimepata fursa ya kuona ndugu zangu waliobaki, wajukuu na mwanangu pekee aliyebakia baada ya wale wanne niliozaa na mke wangu wa kwanza kufariki dunia, sasa nafsi yangu ipo huru nikiamini hata kama Mungu ananichukua nitakuwa itakuwa ni kwa roho nyeupe.

 

“Mke wangu aliyesababisha mimi nikapatwa na masahibu haya naye niliambiwa alishafariki dunia miaka mingi iliyopita, sina kinyongo naye na ninamuombea amani huko alipotangulia nikiamini sisi binadamu sote njia yetu ni moja. Si ajabu hata kesho mimi au wewe tunaweza tukaitwa na Mwenyezi Mungu aliyetuumba.”

 

Anasema mbali na msamaha mkubwa alioupata kutoka kwa Rais Magufuli, anamuomba asiache kumuangalia yeye na wenzake, ikibidi kuwawezesha kwa chochote kutokana na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo na mazingira ya huko kijijini wanakoishi kwa sasa.

 

MWALONGO

Mzee Mwalongo ambaye mwili wake bado unaonekana upo imara licha ya uzee alionao, alisema aliingia gerezani kutokana na kesi ya mauaji akiwa kijana wa umri wa miaka 35 huku akiacha mke na watoto watano wa kuwazaa na mkewe ambaye kwa sasa ni marehemu.

 

“Ukiacha mke wangu, pia watoto wangu watatu nao wamefariki dunia.

“Utaona ni matatizo kiasi gani yameipata familia yangu…ila naamini hii yote ni mipango ya Mungu.”

 

MLYUKA

Kwa upande wake, mzee Mlyuka yeye anasema baada ya hukumu yao walitumikia kifungo hicho katika magereza mbalimbali yakiwemo Isanga, Dodoma, Morogoro, Iringa na Ukonga jijini Dar.

Anasema baada ya kurejea uraiani alikuta wake zake wawili na watoto sita kati ya kumi na mbili wamefariki dunia.

 

“Mambo yamebadilika kabisa, ona nyumbani kwangu kumekuwa ni kama hakuna kitu tena, lakini namshukuru Mungu, pamoja na kwamba wamekufa, lakini nipo uraiani,” anasema mzee huyo.

Wazee hawa na wenzao wengine wawili (jumla watano) walihukumiwa kunyongwa na baadaye kubadilishiwa na kuwa kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya mfanyabishara wa Kihindi.

 

Je, kisa chao kikoje? Usikose mkasa huu mzito wa wazee hawa wiki ijayo kwenye gazeti hilihili la Ijumaa.

Kwa simulizi za sauti na video zao, tembelea Global TV Online kwenye Mtandao wa YouTube kuanzi sasa utakutana na wazee hawa live wakisimulia kilichowapata.

Stori: CATHERINE KAHABI, Ijumaa

Comments are closed.