Benki ya Absa Kuendelea Kudhamini Absa Dar City Marathon
BENKI ya Absa Tanzania imesema itaendelea kudhamini mbio za Absa Dar City Marathon ikiwa kama mdhanini mkuu kutokana na faida za mbio hizo kwa ustawi wa afya za watanzania.
Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizotimua vumbi jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Obedi Laiser alisema kama Absa wanaamini kukimbia kunaleta fursa nyingi katika maisha ikiwa ni pamoja na afya njema jambo muhimu katika ufanisi wa shughuli za uzalishaji mali.
“Katika kukimbia tunajenga afya zetu, ili tuweze kufanya shughuli zetu, tuweze kuishi kwa muda mrefu, ni dhana mojawapo ambayo sisi Absa tunaiishi na ndio maana tukaungana na The Runners Club ili tuweze kuboresha maisha ya watanzania,” alisema Bwana Laiser.
Alisema Absa kama benki kongwe kuliko zote Tanzania ikitoa shughuli za kibenki tokea mwaka 1925 ni imani yao kwa kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo, Klabu ya The Runners mbio hizo zitaendelea kukua na kufikia viwango vya Kimataifa.
“The Runners Club ni wabobezi katika marathon na sisi kama Absa ni wabobezi hasa inapokuja katika utoaji wa huduma bora za kibenki hivyo tunaamini kwa pamoja tunaweza kuifikisha marathon hii mbali zaidi,” alisema mkurugenzi huyo.
Katika mbio hizo Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Runners Club, alisema pamoja na mambo mengine mbio hizo zina malengo ya kutangaza vivutio vya utalii wa Jiji la Dar es Salaam na ndio sababu zilianzia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo na kuzunguuka katika mitaa na barabara mbalimbali maarufu jijini humo.
Zaidi ya wanariadha 3000 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipimana ubavu wakishindana katika mbio za km 21, 10 na 5 huku washindi walikabidhiwa zawadi ya za medali na pesa taslimu.