The House of Favourite Newspapers

BIBI HARUSI AFIA HOTELINI

SIKU za kuaga dunia iliyowekwa na Mungu ikitimia, mja hana hiyari, ataacha vyote na kurejea mavumbini, ndivyo msichana Asha Kilimba (26) ambaye ni bibi harusi mtarajiwa mkazi wa Kinondoni Shamba Jijini Dar, alivyolazimika kuiacha sherehe yake ya ndoa baada ya kukutwa amefariki dunia hotelini.

 

Sababu za kifo chake hazijawekwa wazi na mamlaka za uchunguzi, lakini dada wa marehemu aitwaye Habiba Kilimba alilisimulia Wikienda mwishoni mwa wiki iliyopita mazingira ya kifo cha mdogo wake yalivyokuwa.

 

SIMULIZI HII HAPA

“Mdogo wangu alikuwa afunge ndoa Ijumaa (Agosti 3, mwaka huu) na mchumba wake aitwaye Othman Rashid, lakini ndio limetokea hilo tukio baya.

“Siku ya tukio nilikuwa na marehemu msibani, mjomba wetu alikuwa amefariki dunia, kutokana na msiba huo mdogo wangu alimpigia simu mchumba wake ambaye anaishi Afrika Kusini.

“Mchumba wake alilazimika kuja Dar kushiriki msiba pamoja na kuweka vizuri taratibu za ndoa yao.

“Tulipomaliza taratibu za kusafirisha mwili wa mjomba kwenda Kondoa, (mkoani Singida), mdogo wangu alilazimika kubaki na mchumba wake ili wayajenge mambo yaliyokuwa mbele yao.

“Sisi tukaondoka kwenda Kondoa, nikiwa njiani mdogo wangu alinitumia picha akaniambia yuko kwenye maandalizi ya kwenda kukutana na mchumba wake huyo hoteli ya (jina kapuni), nikamwambia sawa.”

 

KILICHOTOKEA HOTELINI

Baada ya kusimulia hayo, dada huyo wa marehemu alishindwa kuwa na uthibitisho unaoonesha kama ni kweli mdogo wake alikwenda hoteli hiyo kukutana na mchumba wake au mtu mwingine.

Hata hivyo, alieleza kwamba alipomkubalia mdogo wake akakutane na mchumba wake mawasiliano hayakuwepo hadi pale alipopigiwa simu na mmoja wa wahudumu wa hoteli kumtaarifu kuwa Asha alikuwa amefariki dunia.

“Nikiwa msibani Kondoa nikapigiwa simu kuwa mdogo wangu kakutwa hoteli amefariki, nilishtuka sana, utata aliotuachia sisi ndugu ni sababu za kifo chake, hatujui kilichompata.”

 

TAARIFA KUTOKA HOTELINI

Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba marehemu alifika hotelini hapo akiwa na mwanaume ambaye hakujulikana kuwa ndiyo yule mchumba wake au la na kwamba walikodi chumba na kwenda kujipumzisha.

Hata hivyo, mapumziko hayo yalizaa kifo cha bibi harusi huyo mtarajiwa, kilichotokea chumbani hakijafahamika lakini mamlaka za utawala wa hoteli hiyo zinaeleza kwamba mwili wa Asha ulikutwa ukiwa upetapakaa puvu lililotoka mdomoni na puani.

Kuhusu mwanaume aliyekuwa na msichana huyo siku ya tukio, mhudumu wa zamu wa hoteli ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini alisema aliwaona wakati wa kuingia lakini wakati wa kutoka mwanaume huyo hakuonekana.

 

POLISI NA UCHUNGUZI

Dada wa marehemu aliliambia Wikienda kuwa mara baada ya tukio hilo polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi na baadaye kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya maziko ambapo mwili ulisafirishwa hadi Kondoa kwa maziko.

“Mpaka sasa bado tunasubiri uchunguzi, hatujui marehemu alikufaje mle chumbani, lakini ukweli utajulikana kwa sababu damu ya mtu haiwezi kupotea hivihivi,” alisema dada wa marehemu.

 

MCHUMBA ASAKWA

Kufuatia kuwepo kwa madai ya marehemu kwenda hotelini hapo kukutana na mchumba wake, jumba bovu limemwangua mchumba wake huyo na kwamba hatua za kumsaka Othman zimeanza.

“Toka siku ya tukio mimi binafsi sijamuona huyo mchumba, sijui aliko na wala taarifa zake sina.

“Najiuliza ina maana ameshindwa hata kuwasiliana nasi kujua habari za msiba, hii inatia wasiwasi, lakini polisi wametuambia wanamtafuta,” alisema dada huyo.

 

Wikienda lilifika katika hoteli hiyo iliyopo Kariakoo jijini Dar kwa lengo la kwenda kudodosa zaidi kifo cha msichana huyo lakini wahudumu na viongozi wa hoteli waligoma kutoa ushirikiano.

“Unafuatilia hili tukio kwani wewe ni polisi? Polisi ndiyo wenye kazi hii, mimi siwezi kuzumza,” alisema mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo ambaye alitajwa kuwa ni meneja.

Matukio ya watu kufariki dunia wakiwa katika nyumba za kulala wageni yamezidi kujitokeza huku mambo ya kunyongwa, kulishwa sumu, kupatwa na mshtuko wa moyo yakitajwa kuwa chanzo kikubwa cha vifo hivyo.

 

SHEREHE YAFUTWA RASMI

Ndugu wa marehemu wamelazimika kufuta sherehe ya ndoa kutokana na mhusika mmoja kupoteza maisha na mwingine kutokomea kusikojulikana.

“Hakuna ndoa tena, mahari iliyotolewa itabidi busara za familia zitumike maana mchumba mwenyewe haonekani, akionekana ataamua nini kifanyike,” alisema dada huyo wa marehemu.

 

RPC ILALA AJA NA YAKE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamdani pamoja na majibu yake ya mkatomkato alithibitisha kutokea kwa tukio hilo bila kufafanua uchunguzi wa kifo umefikia wapi.

“Wewe si ulikata kujua kama amefia hapo, haya, ni kweli huyo msichana amefia kwenye hoteli hiyo…hayo mengine yaache,” alisema kamanda huyo.

NA NEEMA ADRIAN

Comments are closed.