The House of Favourite Newspapers

Bilionea Subash; Kimbilio La Wanyonge Aliyezimika Kama Mshumaa

0

KIMYA milele! Ule msemo wa Wahenga kwamba kizuri hakidumu, umetimia! Mtu wa watu, binadamu mwenye moyo wa kipekee kabisa, anayezibeba shida za wengine kama za kwake, anayetatua matatizo makubwa ya watu kimyakimya bila kutangaza popote, Subash Patel, amekwenda!

 

Jumanne ya Disemba 15 asubuhi, ndipo mtu huyu wa watu alipotwaliwa! Taarifa zilipoanza kusambaa kwamba Subash Patel hatupo naye tena, baada ya kufikwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mfupi, mioyo ya watu wanaomfahamu au waliofaidika na moyo wake wa upendo, iligubikwa na majonzi mazito.

 

Rais Dk John Magufuli anahuzunika, yule mshirika wake mkubwa katika kuelekea Tanzania ya Viwanda, ambaye kwa zaidi ya miongo kadhaa amekuwa mwenyekiti wa wamiliki wa viwanda Tanzania, amekwenda.

Wafanyabiashara wakubwa nchini wanalia, wamiliki wa viwanda nchini wanalia, wafanyabiashara wadogo wanalia, maelfu ya Watanzania walioajiriwa kwenye kampuni zake pamoja na wategemezi wao wote wanalia, hakika Tanzania imezizima kufuatia kuanguka kwa mbuyu huu, Subash Patel, miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa na utajiri mkubwa kabisa nchini.

SUBASH PATEL NI NANI?

Kwa kumtazama unaweza kudhani kwamba ni Mhindi kutoka barani Asia lakini ukweli ni kwamba Subash Patel ni mtanzania halisi, alizaliwa Agosti 13, 1946 katika kijiji kidogo cha Lugoba mkoani Pwani na kupewa jina la Subhashbhai Mothibai Patel.Baadaye baba yake Motibhai Patel na familia yake ikahamia Ngerengere, Morogoro kabla ya kuja kuweka makazi ya kudumu jijini Dar es Salaam.


Katika moja ya mahojiano aliyoyafanya enzi za uhai wake Subash anasema babu zake walihamia Tanzania miaka mingi nyuma wakitokea India, akazaliwa baba yake hapahapa nchini kisha akazaliwa yeye na yeye akazaa watoto ambao nao wamemletea wajukuu, kwa hiyo ni Mtanzania anayejivunia Utanzania wake bila kujali asili ya India aliyonayo.Licha ya utajiri mkubwa uliokuwepo kwenye familia yao, Subash hakuwa mvivu wa shule na hiyo ikamfanya kuwa miongoni mwa wasome wa mwanzomwanzo nchini Tanzania.

 

Mwaka 1968, alihitimu shahada ya uhandisi wa umeme, Bachelor Degree in Electrical Engineering aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza.Mwaka 1971 akapata shahada ya pili (masters) katika masomo hayohayo ya uhandisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Brunel jijini London nchini Uingereza.

 

Katika kipindi hicho alipokuwa anasoma nchini Uingereza, Patel pia alikuwa anafanya kazi na Plessey Telecommunication Research Ltd yenye makao makuu yake Maidenhead kuanzia mwaka 1968 mpaka 1971.Baadaye alijiunga na Kampuni ya Bell- Northern Research, Ottawa nchini Canada hadi mwaka 1977 alipoamua kurejea nchini na kusimamia biashara za baba yake, Motibhai Patel.

 

SAFARI YA MAFANIKIO

Kwa hapa nchini, safari ya mafanikio ya Subash, ilianza mwaka 1992 baada ya kushirikiana na baba yake, Motibhai Patel fungua kampuni ya Motisun Group jijini Dar es Salaam, ambayo ilikuwa ikimiliki kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za chuma ikiwemo nondo na mabati.Huo ulikuwa mwanzo tu, kiwanda hicho kikazidi kutanuka na kuwa kikubwa zaidi, kikaongeza uzalishaji pamoja na uwekezaji wake na kama ulikuwa hujui, kiwanda hicho ndiyo kile ambacho kwa sasa kinajulikana kama MMI Steel, kilichopo Mikocheni, Barabara ya Motisun.Huo ulikuwa mwanzo tu wa mafanikio, Subash aliendelea kuwekeza kwa nguvu kwenye sekta ya viwanda na baadaye akaja kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wenye Viwanda Tanzania (CTI), inayoundwa na zaidi ya wamiliki wa viwanda 400 nchini.

 

UWEZEKAJI MKUBWA

Subash aliendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania kwa kufungua viwanda mbalimbali. Akaanzisha kiwanda kingine cha uzalishaji wa vinywaji baridi cha Sayona na kwa taarifa yako tu, Sayona ndiyo waliokuwa wa kwanza nchini kuzalisha vinywaji baridi katika chupa za plastiki, kikiwa na matawi katika maeneo kadhaa nchini.Subash hakuishia huko, aliamua kufungua viwanda vingine vya kusindika matunda, cha kwanza kikiwa ni katika Kijiji cha Mboga, Kibaha mkoani Pwani ambacho kazi yake kubwa ni kusindika mbogamboga na matunda kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao kwa wakulima.

 

Kiwanda hiki kimeleta ahueni kubwa kwa maelfu ya wakulima, ambao awali matunda yao yalikuwa yakiozea shambani kutokana na kukosa masoko lakini sasa, kiwanda kinanunua matunda yote kwa wakulima na bado hayatoshi.

 

Uwekezaji wa Subash haujaishia hapo, amewekeza pia katika viwanda vingine, vikiwemo vya uzalishaji wa saruji ya Chapa Kiboko, uzalishaji wa rangi mbalimbali za majumbani na viwandani sambamba na uzalishaji wa matanki makubwa ya kuhifadhia maji chapa ya Kiboko.

 

Kwenye upande wa utalii pia Subash hakuwa nyuma, amewekeza kwenye ujenzi wa mahoteli makubwa na ya kisasa yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano, yakiwemo White Sands na Seacliff za jijini Dar es Salaam na Zanzibar.Hoteli hizi zinasifika kwa ubora wake na watu mashuhuri kutoka mataifa makubwa wanaokuja kutembelea Tanzania na Afrika Mashariki, wamekuwa wakifikia kwenye hoteli hizi.

 

UHUSIANO WAKE NA RAIS MAGUFULI

Jitihada zake za kuwekeza nchini kwa kuanzisha viwanda vinavyotoa ajira kwa maelfu ya wazawa, zilimfanya Subash kuwa kipenzi cha Rais Magufuli ambapo mara kadhaa amekuwa akimsifu hadharani na kuwataka matajiri na wawekezaji wengine kuiga mfano wake kwa jinsi anavyojitoa kuhakikisha Tanzania ya Viwanda inawezekana.

 

Katika matukio yatakayokumbukwa, ni pamoja na Mhe. Magufuli alipoenda kufungua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona kilichopo Nyakato Mjini Mwanza, kilichojengwa na Subash kupitia kampuni yake ya Motisun kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 11 na Milioni 800 ambapo mheshimiwa rais alimsifu hadharani kwa uwekezaji huo.“

 

Bw. Subhash nakupongeza sana, wewe jenga viwanda Serikali itakuunga mkono, na nataka niwaambie wafanyabiashara na wawekezaji, huu ndio wakati wa kuwekeza na mimi nawapenda wafanyabiashara na wawekezaji, hapa kusingekuwa na kiwanda hiki, vijana hawa 200 wasingepata ajira, nataka kukupongeza sana hata kwa mpango wako wa kujenga viwanda vingine vitano mwakani, hii ni safi sana.”

 

JINSI ALIVYOKUWA AKIJITOA KUISAIDIA JAMII

Miongoni mwa watu waliokuwa na mioyo ya kipekee ya kusaidia jamii, ni Subash Patel na alikuwa akiutumia vyema msemo kwamba ukitoa kitu kwa mkono wa kulia kumsaidia mtu, hata mkono wako wa kushoto hautakiwi kujua.

 

Kila aliyefanikiwa kuonana na Subash enzi za uhai wake na kumweleza matatizo yake, alikuwa akisaidiwa kwa moyo mkunjufu na zipo shuhuda za kutosha za watu mbalimbali ambao walisaidiwa na mtu huyu aliyekuwa na moyo wa kipekee.Utajiri wake mkubwa kamwe haukumfanya ajikweze na kuwaona wengine kama hawana maana, mara zote alikuwa nuru ya wale waliokuwa gizani.

 

Ni mara chache sana ndipo ungeweza kumsikia Subash akitangazwa hadharani kwamba ametoa msaada, jambo ambalo watu wanaomjua vyema wanaeleza kwamba hakuwa akilifurahia! Alipenda zaidi kusaidia watu bila watu wengine kujua!

 

Moyo wa kipekee kabisa.Wakati wa janga la ugonjwa wa Corona, Subash alikuwa miongoni mwa watu waliounga mkono juhudi za serikali kupambana na ugonjwa huo ambapo alitoa jumla ya matanki ya kuhifadhia maji ya kunawia mikono 1000, na aliyekuwa waziri wa Afya kipindi hicho, Ummy Mwalimu ndiye aliyepokea msaada huo.

 

Hilo lilikuwa miongoni mwa matukio adimu ya Subash kuonekana hadharani akiisaidia jamii lakini kiuhalisia, anaweza kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiongoza kuisaidia jamii kwa wingi pamoja serikali kwa jumla.

 

MAZISHI YAKE

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia yake, Subash anatarajiwa kufanyiwa ibada ya mazishi katika Hekalu la Baps la Wabudha, lililopo Mtaa wa Pramukh Swami, Upanga jijini Dar es Salaam.Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina

MAKALA: MWANDISHI WETU | GPL

Leave A Reply