The House of Favourite Newspapers

Binti kutoka Moshi adaiwa kunyongwa!

0

DAR ES SALAAM: Tangulia! Mwili wa binti Theresia John ,16, (pichani) aliyekuwa akiishi Tegeta Azania jijini hapa aliyekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga, umezidi kuleta utata baada ya ndugu zake kudai kuwa, mtoto wao hakujinyonga bali alinyongwa.

Akizungumza na waandishi wetu, mama wa marehemu,  Dafosa Lukaa alisema:
“Theresia aliondoka Oktoba, mwaka 2015 nyumbani kwao,  Moshi, Kilimanjaro na kutua Dar kwa ajili ya kufanya kazi kwenye duka lililopo Kariakoo.

“Mwanangu alipofika Dar alipokelewa na mama mmoja aliyefahamika kwa jina la mama Luka ambaye ndiye aliyemuita na kumpeleka kwa ndugu yake anayeishi Tegeta kwa ajili ya kazi za ndani,” alisema.

Hata hivyo, mama huyo anakiri kutowafahamu watu waliomchukua mtoto wake japo kwa sura na hata baada ya kutokea kwa taarifa ya msiba na wao kuja Dar, watu hao hawaoneshi ushirikiano wowote.

“Aliondoka Moshi na kuja Dar kwa ajili ya kufanya kazi lakini baada ya siku chache kabla ya kifo chake alianza kuwapigia ndugu zake simu akiwaambia baba mwenye nyumba anamnyanyasa ila mama mwenye nyumba hana tatizo naye.

“Siku ya pili akanipigia tena simu na kudai kuwa amechoka kufanya kazi hapo kwani baba mwenye nyumba amezidi kumnyanyasa na anataka kurudi nyumbani Moshi kwani anamnyima amani kwa kumfokea na kumuahidi kuwa atakula naye sahani moja.

“Nakumbuka mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa Jumapili, nikamwambia namfanyia mpango ili arudi nyumbani cha ajabu Jumatatu (kesho yake) nikapata taarifa  kuwa amejinyonga, hata siamini kwani mazingira ya kifo chake ni ya kutatanisha mno, huenda kanyongwa, naomba vyombo husika vitende haki kwa damu ya mwanangu,” alisema mama huyo.
Kufuatia kifo hicho kilichoacha viulizo kwenye familia ya marehemu, mwili wake ulisafirishwa kwenda kijijini kwao Moshi na kuzikwa Jumanne.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime amekiri kupokea taarifa za tukio hilo na kusema kuwa, kwa mujibu wa vielelezo vya uchunguzi wa polisi inaonekana kuwa binti huyo alijinyonga.

“Mwili wa marehemu una kila dalili za mtu aliyejinyonga ila ndugu zake hawataki kuamini hivyo imebidi mwili ufanyiwe uchunguzi wa kitabibu kwa hiyo tunasubiri majibu,” alisema.

Leave A Reply