The House of Favourite Newspapers

Bomoabomoa Dar yaacha vifo, vilio

0

_DSC0011Muhanga wa bomoabomoa hiyo akiongea kwa uchungu.

Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Zoezi la bomoaboa ambalo limeikumba Jiji la Dar es Salaam kwa karibu mwezi mmoja sasa na kusitishwa hivi karibuni, limeacha vilio na kusababisha vifo huku mazito zaidi yakiibuka, Uwazi lina ripoti ndefu.

Wiki iliyopita, timu ya Uwazi iliingia mitaani katika maeneo mbalimbali ya jiji yaliyokumbwa na zoezi hilo na kufanya mahojiano na baadhi ya wafiwa na wananchi pia viongozi wa serikali za mitaa ambapo wengine walisema zoezi hilo lilikuwa gumu na kuishukuru serikali kwa kutambua hilo na kuamua kusitisha licha ya kwamba kuna waliobaki yatima na wajane.

HUYU ALIFARIKI KWA MSHTUKO
Hussein Jovit (26), mtoto wa marehemu Jovit Hussein Kobelo (54), ameliambia Uwazi hivi karibuni kwamba baba yake alifariki dunia saa 2:45 usiku wa Desemba 21, mwaka jana kwenye Hospitali ya Mwananyamala ambako alikimbizwa kwa matibabu.

IMG_1349

Moja ya familia iliyokumbwa na sekeseke hilo.

ANASIMULIA
“Siku hiyo, kwenye saa 10:30 jioni, baba alitoka kwa mama mdogo (mke mdogo), Kinondoni Hananasif ambaye nyumba yake ilibomolewa. Sasa wakati akija kwa mama (mke mkubwa) Kinondoni Mkwajuni kujihifadhi, akakuta tingatinga likibomoa nyumba yetu. Palepale akadondoka kwa mshituko na hakuwahi kusema neno lolote.

“Tulichokifanya ni kumkimbiza Mwananyamala kwa matibabu lakini akafariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.


“Tuliandaa mazishi, tulisafirisha mwili kwenda kumzika Morogoro. Kwa sasa familia imesambaratika, watoto wengine tumepewa hifadhi na wasamaria wema.”
“Baba alijenga nyumba hizi kipindi cha nyuma. Hakuna aliyefahamu kuwa kuna siku zitakuja kubomolewa na kusababisha kifo chake.”

HUYU AMEPOTEZA MAMA
Peter Chiwalo, mkazi wa Kinondoni Hananasif jijini Dar, alisema bomoabomoa iliwahi kuwakumba mwaka 2012 ambapo nyumba zao tano zilibomolewa na kubakiwa na kibanda, yeye alipata mshtuko na kulazwa hospitalini.

bomoa-1

Muonekano wa makazi yaliyobomolewa.

“Mama yangu, Angela Ally Lukama naye akawa anaumwa. Wiki mbili zilizopita (Desemba 28, 2015), alisikia kuna bomoabomoa nyingine inakuja, akapata mshtuko na kufariki dunia,” alisema kwa uchungu Peter.

MJUMBE SERIKALI YA MTAA ASIMULIA
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kawawa, Kinondoni, Steven Gwakava yeye alisema katika eneo lake, mzee Juma Mohammed Mwalome (68) amepoteza mtoto mmoja, Mohammed Juma kwa mshtuko baada ya kusikia nyumba ya baba yake imebomolewa. Marehemu huyo alipata habari hizo akiwa Morogoro na kufia hukohuko.

MRATIBU WA MITAA 18 AONGEA NA UWAZI
Naye Mratibu wa Muungano wa Mitaa 18 katika Bonde la Mto Msimbazi, Godwin Cuthbert alisema:

“Katika eneo langu watu wamepoteza maisha na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wamepatwa na mshtuko kutokana na nyumba zao kubomolewa wakati baadhi yao wana hati za kumiliki kihalali.”

indexeeeUWAZI LAFIKA MTAA WA SUNA, MAGOMENI
Salum Hamis (pichani) ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Suna, Magomeni Mapipa, yeye alipata mshtuko na kupoteza fahamu kufuatia nyumba yake kubomolewa.

Anasema: “Ilikuwa Januari 5, mwaka huu. Siku hiyo nilikuwa natoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi kusikiliza kesi ya pingamizi la kubomolewa nyumba yangu. Kufika nyumbani sikuikuta, ilishasambaratishwa na tingatinga. Nilijisikia vibaya, nikaanguka na kupoteza fahamu.

“Nilipelekwa zahanati moja ya hapahapa Magomeni ambako nilipatiwa matibabu. Sasa hivi najisikia nafuu kidogo na kuna hizi dawa naendelea kutumia. Kwa sasa naishi kwa ndugu yangu maeneo hayahaya.”

IMG-20160109-WA0000

Marehemu Jovit Kobelo enzi za uhai wake.

MAMA ANAISHI NJE NA FAMILIA
Fatuma Mustafa ni mama wa watoto wanne na wajukuu watatu. Yeye alikuwa akiishi kwenye nyumba ya urithi ya baba yake iliyojengwa mwaka 1973. Nyumba hiyo imebomolewa wiki iliyopita na ameshindwa kupata mahali pa kwenda hivyo kuendelea na maisha eneo alilovunjiwa. Mume wake yuko Wilaya ya Rufiji, Pwani akijiuguza kwa ugonjwa ambao hakuuweka wazi.

“Naishi kwa tabu na watoto hawa kwani sina kazi, kula kwangu mpaka nifanye kibarua cha kuwafulia nguo watu na wakati mwingine nakosa na kulala na njaa. Je, hizo pesa za kupangia chumba nitazipata wapi?” alihoji mama huyo.

UONGOZI WAVURUGIKA
Baadhi ya watu walioathirika na bomoabomoa hiyo walisema kuwa baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa Magomeni waliobomolewa nyumba zao wamehamia Mbagala, Dar hivyo kukosa sifa za kuongoza mitaa hiyo.

TAMKO LA SERIKALI
Wakati hali ikiwa hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, serikali ilitoa tamko la kusitisha bomoabomoa katika baadhi ya maeneo hatarishi jijini Dar isipokuwa kwa nyumba zilizopo kwenye Bonde la Mto Msimbazi ambapo oparesheni hiyo itaendelea.
Pia, serikali kwa kuthamini wananchi wake, imesema itawafidia na kuwatafutia makazi wale wote wenye vielelezo vinavyowaruhusu kuishi katika maeneo hayo.

IMG-20160109-WA0001

Kaburi alilozikwa marehemu Jovit.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Januari Makamba alisema kusitishwa kwa operesheni hiyo kunapisha uhakiki mpya wa baadhi ya nyumba zilizowekewa alama ya X wakati maeneo hayo yameidhinishwa na mamlaka za serikali.
Waziri Makamba alisema zoezi la kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni lipo kisheria ingawa kuna baadhi ya kasoro ambazo zilijitokeza katika utekelezaji wake.

SERIKALI HAITESI WANANCHI
Waziri huyo alisema serikali ya awamu ya tano haiko kwa ajili ya kuwatesa wananchi wake, hasa wanaofuata sheria ndiyo maana mawaziri wanaohusika walikaa meza moja na kuamua kuangaliwa upya kwa oparesheni hiyo.

WALIOSIMAMIA ZOEZI VIBAYA KUKIONA
Pia, Makamba aliweka wazi mpango wa serikali wa kuwachukulia hatua watendaji wote waliosimamia oparesheni hiyo kwa kukiuka taratibu na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Tangu Desemba 17, mwaka jana mpaka wiki iliyopita, nyumba 774 zimeshabomolewa jijini Dar huku nyingine zikiwa kwenye zuio la Mahakama ya Ardhi.

Leave A Reply