The House of Favourite Newspapers

Bongo Muvi mmelala, amkeni!

0

KWENU mastaa wa sinema za Kibongo. Nawasalimu kwa umoja wenu. Vipi wazima wote? Poleni na majukumu ya kila siku, naamini mnaendelea kupambana, Mungu ni mwema, abariki kazi za mikono yenu kila siku.

Mkitaka kunijulia hali mimi ndugu yenu, sijambo. Namsukuru Mungu naendelea kupambana katika eneo langu, maisha yanazidi kusogea. Namshukuru Mungu kwa kunijalia uzima na afya, naendelea kuwahabarisha Watanzania.

Nimewakumbuka leo kwa mara nyingine ndugu zangu. Nimewakumbuka baada ya wiki iliyopita kukutana na wadau wa sinema na kuzungumza nao mawili matatu. Nao walikuwa na mtazamo kama wangu juu ya mwamko wenu katika kazi yenu.

Ndugu zangu, ninaposema mmelala haimaanishi kwamba hamfanyi kazi lakini kwa kuwa nipo katika tasnia hii ya burudani kwa zaidi ya miaka sita sasa, naona tunakoelekea siko. Siku hizi sioni zile ‘vurugu’ za mara kwa mara zinazohusu wasanii wa filamu.

Kila nikiamka nasikia, Diamond kafanya hivi, Alikiba kafanya vile. Kifupi Muziki wa Bongo Fleva unateka soko la burudani kwa sasa. Naona namna ambavyo wasanii wa Bongo Fleva wanavyovuka mipaka kwenda nje kufanya video zao kali kwa gharama kubwa.

Nawaona jinsi wanavyochuana kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa nje ya nchi katika nyimbo zao. Sasa hivi si Nigeria tu, wamevuka mipaka hadi katika ardhi ya Obama, wanawashirikisha Wamarekani katika kazi zao.

Lakini Bongo Muvi sisikii. Sioni jitihada zenu katika eneo la kimataifa. Mnaonekana kama mmeridhika na soko la ndani. Siwaoni hata mkifanya matamasha makubwa ya sinema. Sioni mkizindua sinema zenu mpya ambazo zinaingia sokoni.

Siwaoni mkivuka mipaka kama vile alivyoanzisha marehemu Steven Kanumba kwa kuwashirikisha wasanii wakubwa kutoka Nigeria. Ni kama alikufa na tasnia yake. Alipokuwa hai tuliona ushindani. Mlijituma sana na Watanzania wakawa wanapata vitu vizuri.

Ilikuwa tunasikia leo msanii huyu anatoa sinema mpya, kesho unasikia mwingine anatoa. Habari zenu katika magazeti ya Global Publishers ndizo zilikuwa zikitawala. Kwa sasa kama vile hampo. Nini kinaleta shida?

Mbona vifaa na wasanii wenye uwezo wa kufanya makubwa wapo? Mbona baadhi yenu mlikuwa mahiri sana kipindi cha nyuma na kumfanya Kanumba asilale usingizi kutokana na ushindani mliokuwa mnauonesha lakini kwa sasa mmepoa.

Wadau wa kuwasapoti wapo. Wapeni ‘proposal’ za kazi zenu, watawadhamini na mtafanya kazi mbalimbali ambazo zitavuka mipaka. Tunataka kuona na nyinyi mnashirikiana na wasanii wa kimataifa.

Tunataka kuona na wao wanakimbizana kuja nchini kuwaomba kufanya kazi na nyie. Watanzania wanawaamini, piganeni muweze kuwapa raha.

Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa. Naomba mfanyie kazi ushauri wangu na mrudi kwenye soko kama zamani.

Mimi ni ndugu yenu;

Erick Evarist

Leave A Reply