The House of Favourite Newspapers

Bosi Simba Atoa Tamko baada ya kichapo cha mabao 5-1 Dhidi ya Yanga

0
AHMED Ally ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba.

AHMED Ally ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, ameibuka na kuwataka mashabiki wa timu hiyo, kuwa wavumilivu kwa kuwapa muda viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kujitatahimini baada ya kichapo cha mabao 5-1.

Simba ilikutana na kichapo hicho katika mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga uliopigwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Kennedy Musonda, Stephene Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli aliyepachika mawili, huku Kibu Denis akipachika la kufutia machozi upande wa Simba.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ally alisema kuwa ipo namna ya  mashabiki kujua sababu ya kipigo hicho kikubwa cha mabao 5-1 walichokipata katika dabi hiyo.

Ally alisema wakati wakisubiria sababu hizo za kipigo, mashabiki wanatakiwa kuvumilia, huku wakielekeza nguvu katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara watakaocheza dhidi ya Namungo FC.

Aliongeza kuwa, hawatakiwi kutoka mchezoni, badala yake mashibiki waendelee kuisapoti timu kwa kujitokeza uwanjani katika mchezo ujao ambao ni muhimu kwao kupata ushindi.

“Kwenye mkutano wa Wanahabari nilisema, hii ni mechi ambayo matokeo yake hua yanaacha furaha ya kudumu au huacha maumivu ya kudumu kwenye mioyo ya mashabiki.

“Kwa bahati mbaya ni sisi ndio tumebaki na maumivu ya kudumu, kila MwanaSimba anawaza sababu tafauti tofauti iliyosababisha tupoteze mchezo huu muhimu kwetu kupata ushindi.

“Hivyo namna sahihi ya kujua sababu hizo nayo ni utulivu, kikubwa tuwape viongozi, Benchi la Ufundi na wachezaji wetu utulivu wa kujitathmini kwa maslahi ya mechi zijazo

“Novemba 9, kuna mchezo dhidi ya Namungo hivyo ni vema tukajikita zaidi kuangalia tunachukuaje alama tatu hizo baada ya kupoteza dhidi ya Yanga,” alisema Ally.

STORI NA WILBERT MOLANDI NA ISSA LIPONDA

Leave A Reply