The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Dkt. Mwinyi Ashinda Urais Zanzibar – Video

0

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imemtangaza mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi kuwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote.

 

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahamoud Hamid amesema wagombea urais walikuwa 17 waliopigiwa kura 498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha.

 

Amesema kura zilizoharibika zilikuwa 10,944 sawa na asilimia 2.19; “Kwa mujibu wa kifungu cha 96 (2 na 3) ya Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya 2018, namtangaza rasmi Dk Hussein Ally Mwinyi wa CCM kuwa amechaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020,” amesema.

 

Jaji Hamid amesema ZEC imehakiki matokeo ya wagombea wote wa Zanzibar na kujiridhisha kuwa yako sahihi. Amesema mgombea anayefuatia ni Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

 

Baada ya kutangazwa mshindi Dkt.Mwinyi amesema “Nimepokea ushindi kwa mikono miwili, Nashukuru kuwa wananchi walio wengi wamenichagua mimi na chama changu cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo.

 

Nawashukuru kwa uvumilivu na ustahamilivu mkuwa. Niwashukuru zaidi kwa kunipigia kura za kutosheleza kuwa rasi wa Zanzibar. Nitalipa imani hii kwa utumishi uliotukuka,” Dkt Mwinyi amesema.

 

Dkt.Mwinyi aliongeza kusema Zanzibar mpya itajengwa na Wazanzibari wote bila kujali itikadi , Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofuati zao.

 

“Mimi Hussein Mwinyi si bora kuliko CCM ushindi huu ni wa wana Wazanzibari wote ,uchaguzi sasa umekwisha turudi kujenga Zanzibar mpya.

 

Aidha amesisitiza wafuasi wa CCM ,washeherekee kwa ustaha bila kukwaza wengine kwa kuwa ushindi wasingepata pasipo kuwa na ushindani.

 

Ushindi huu umetangazwa wakati Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye ni mgombea wa urais visiwani Zanzibar, Maalim Seif Seif Sharif Hamad akiwa amekamatwa kwa mara pili.

 

Maalim Seif alikamatwa muda mfupi baada ya kutangaza kuongoza maandamano ya amani. Siku ya Jumanne Maalim Seif alikamatwa katika kituo cha kupigia kura cha mtoni Garagara na na kupelekwa makao makuu ya polisi kisiwani Zanzibar ambako aliachiliwa saa kadhaa baadaye katika hatua ambayo ilishutumiwa vikali na viongozi wa upinzani.

 

Leave A Reply