The House of Favourite Newspapers

Breaking News: Lugola Awasili TAKUKURU Kuhojiwa

0

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) makao makuu jijini Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa.

 

Lugola amefika katika ofisi hizo leo Ijumaa Januari 30, 2020, saa 1.24 asubuhi akiwa katika gari ndogo aina ya Klugger rangi nyeusi na hakuingia nayo ndani ya geti.

 

Akiwa amevalia kaunda suti nyeusi huku mkono wa kulia akiwa ameshika iIlani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mkoba mweusi, alionekana mwenye kujiamini zaidi na akielekea moja kwa moja eneo la mapokezi ndani ya jengo hilo lililoko mtaa wa Jamhuri.

 

Mmoja wa maofisa wa Takukuru alimwongoza kuingia ndani ya jengo ambako alikwenda kukaa eneo la mapokezi mahali walipokuwa wamekaa waandishi na wakatakiwa kumpisha.

“Hata ninyi mpo huku?  Oh! hata wewe nawe upo!  Haya, hamjambo, habari zenu!” alisalimia Lugola akipunga mkono uliobeba ilani ya CCM.

 

Mmoja wa maofisa wa Takukuru alisema baada ya Lugola kuhojiwa, saa 3.30 angehojiwa aliyekuwa Kamishina wa Zimamoto, Thobias Andengenye, saa 8.00 angehojiwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Jakob Kingu,  ambaye sasa ni balozi na saa 12 jioni angehojiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

 

Kuhojiwa kwa watumishi hao ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuhusu mkataba tata walioingia katika manunuzi ya vifaa vya zimamoto.

Leave A Reply