The House of Favourite Newspapers

Vyama Vya Upinzani Vyamvaa Jaji Mutungi – Video

Vyama 10 vya upinzani nchini vimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kurejesha ratiba za vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa ili kupata fursa ya kujadili Muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge.

 

Akizungumza leo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kikao cha kamati ya uongozi ya baraza kilichoketi Desemba 4, 2018, wajumbe walikubaliana Desemba 21 na 22, 2018 kifanyike kikao kujadili muswada huo.

Vyama hivyo ni ACT-Wazalendo, ADC, CCK, Chaumma, CUF, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi, NLD na UPDP.

Muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni ambako Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai ataipangia Kamati ya Bunge itakayofanya uchambuzi.

Mwalimu amesema kupitia kikao hicho  vyama vya siasa  vingepata fursa ya kuupitia na kujadili muswada husika na kisha kutoa msimamo wa pamoja wa baraza hilo.

Amesema wanashangazwa na uamuzi wa Msajili kwa maelezo kuwa ameahirisha kikao hicho na kukwamisha lengo lao la kujiandaa kutumia fursa hiyo kuzungumzia muswada huo aliodai kuwa ni kandamizi.

Mwalimu amesema Msajili hakushauriana na Kamati ya uongozi ya Baraza na kufikia uamuzi wa kuahirisha kikao hicho.

“Hakushauriana na wala hakukuwepo na kikao cha kamati ya Baraza la uongozi. Uamuzi wa kuahirisha  umefanywa na msajili kwa kushirikiana na watu wake,” amesema Mwalimu.

Kifungu cha 19 kinapendekezwa kurekebishwa ili kumwezesha msajili wa vyama vya siasa kufuta usajili wa chama cha siasa kitakachobainika kuwa kilipata usajili kwa njia zisizo za halali.

Muswada huo unalenga katika kuzuia viongozi wa vyama vya siasa kutokuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini.

 

Comments are closed.