The House of Favourite Newspapers

Bunge Lilivyopitisha Bajeti Itekelezwe Ilivyo

0

 

Stori: Eric Shigongo| Uwazi | Napasua Jipu

ALHAMISI ya wiki iliyopita serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango iliwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2017/18, ambayo ni ya pili tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie maradakani.

Bajeti hii ni kama ilivyokuwa ya mwaka wa fedha uliopita, ni nzuri kwa sababu imeonyesha matumaini kwa Watanzania kwa sababu fedha nyingi zimeelekezwa kwenye shughuli za maendeleo.

Lazima tukiri kwamba tangu Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani kumekuwa na mabadiliko ya wazi kwamba shughuli za maendeleo zinaonekana wakati miaka ya nyuma fedha nyingi zilikuwa zinapangiwa matumizi ya kawaida, kwa maana ya posho, chai, wageni na semina mbalimbali.

Bado kuna kipengele cha kuijadili na kuipitisha, kazi ambayo ni ya wabunge na kuitekeleza ni kazi ya watumishi wa serikali, lakini wabunge wakumbuke kuwa wana kazi nyingine ya kusimamia kile watakachoamua kuwa kwa sababu wao ni wawakilishi wa wananchi.

Nasema hivyo kwa sababu utekelezaji wa bajeti na usimamizi huwa ni tatizo sugu na hudhihirishwa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali inapotoa taarifa yake baada ya kukagua mahesabu ya fedha za serikali.

Kwa kuwa Serikali ya Magufuli inapambana na rushwa na kila aina ya ubadhirifu wa fedha za umma, nina imani kwamba utekelezaji na matumizi ya fedha zitakazopitishwa ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 31, utakuwa ni wamanufaa kwa wananchi wote wa nchi hii.

Niwakumbushe wabunge kwamba kilio cha wananchi miaka nenda rudi ni kwamba, fedha zinazotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo huwa ni ndogo kama vile kutekeleza miradi ya maendeleo wanadai ni pungufu ya asilimia 50 ya fedha zilizopitishwa na Bunge.

Nimejitahidi kufuatilia mijadala ya wizara mbalimbali tangu mkutano huu uanze na kubaini kuwepo malalamiko ya baadhi ya wabunge kuwa fedha nyingi zilizotengwa na Bunge kutopelekwa katika maeneo husika.

Tumewahi kumsikia Rais Magufuli akishangazwa na baadhi ya wizara kudaiwa mabilioni ya shilingi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) au taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji. Kiongozi wa nchi ilibidi ahoji, kwa nini hawalipwi wakati Bajeti ya Serikali inatenga fedha?

Wabunge ni lazima wahakikishe fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo sehemu fulani, zinafika na kufanya kazi husika.

Ni wazi usimamizi wa fedha za umma ukiwa mzuri, hata Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) hatutaona akionesha fedha za umma zinavyotafunwa na wenzetu wachache na upungufu anaouonesha kila mwaka katika utunzaji wa fedha za umma.

Sisi wote ni mashahidi kwamba kwa miaka mingi iliyopita hata ya mwaka jana, ripoti ya CAG ilionyesha namna ya fedha za umma zilivyochotwa, jambo ambalo wapenda maendeleo na wazalendoi wa nchi hii hawataki litokee tena katika bajeti hii.

Katika ripoti yake kuhusiana na bajeti ya mwaka jana, CAG aligundua kuhamishwa kwa fedha zilizopangwa kwa ajili ya eneo fulani zikapelekwa eneo lingine, jambo ambalo wabunge wamelipigia kelele sana bungeni.

Naamini bajeti iliyowasilishwa wiki iliyopita na ambayo itajadiliwa wiki hii na wabunge, itapunguza manung’uniko hayo ya kila mara na kuweka misingi imara ya utekelezaji itakayolingana na vipaumbele vitakavyoidhinishwa na Bunge na wahusika wataheshimu maamuzi ya wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.

Kuamua vinginevyo tofauti na uamuzi wa Bunge uliopitisha mipango yote ya matumizi ya fedha hizo, kifungu kwa kifungu ni kulifanya Bunge kutokuwa na umuhimu wowote licha ya ukweli kwamba wanajadiliana vizuri na kutumia muda mrefu huku fedha za umma zikitumika wakati baadhi ya watu hawaheshimu uamuzi wa Bunge.

Narudia, watekelezaji wa bajeti ambao wana dhamana, hawana budi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo za umma ili zitumike kama ilivyopangwa na wabunge badala ya kuishia kwenye mifuko ya wachache na kuacha wananchi wakitaabika kwa kukosa miundombinu, huduma za matibabu na shule pamoja na walimu wanaolalamikia mafao yao kila mwaka.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply