The House of Favourite Newspapers

BUSARA ZA UHURU KENYATTA ZIMEITIKISA SAFARI YA CANAAN

0

BUSARA ZA UHURU KENYATTA

 

 

JANA huko nchini Kenya, kumetokea tukio lisilo la kawaida kwa watawala. Uhuru Kenyatta ameyaheshimu maamuzi ya mahakama yaliyofutilia mbali uchaguzi na kuutaka urudiwe baada ya siku 60.

 

Si jambo la kawaida kukubaliana na maamuzi ya mahakama, lakini kwa Kenyatta ameonesha ukomavu mkubwa wa nafsi, mwili, akili, kisiasa na kidemokrasia. Kaacha fikra zake na hisia za kibinadamu kuwa labda huenda mahakama haikumtendea haki, akaamua kukubaliana na maamuzi hayo kwa manufaa ya Wakenya. Hii ni hatua kubwa inayostahili pongezi.

 

Mahakama kama mhimili wa serikali, haupaswi kuingiliwa kwa namna yoyote ile, mhimili huu hutakiwa kufanya kazi kwa uhuru bila kupokea ‘maagizo kutoka juu,’ hivyo, mahakama kuu nchini Kenya inastahili kongole.

 

KUHUSU SAFARI YA CANAAN

Kaulimbiu hii inatumiwa na Raila Odinga. Mara baada ya matokeo kutangazwa kuwa ameshindwa katika uchaguzi, alipinga waziwazi kuwa, matokeo hayo yaligubikwa na mizengwe mingi iliyochezwa ili kumuibia kura zake. Matumaini ya kuendelea na safari ya ‘Canaan’ yakahamia mahakamani ambako ndiko haki ilikopatikana.

 

Ni maamuzi haya ya mahakama ndiyo yanampa nguvu Odinga kujinadi kuwa, ‘Safari ya Canaan haizuiliki tena’ Moto umewashwa!

 

NANI KUIBUKA KIDEDEA?

Mchuano ni mkali mara mbili zaidi ya ulivyokuwa. Busara iliyoonyeshwa na Uhuru Kenyatta ya kuamua kukubaliana na maamuzi ya mahakama na kusisitiza amani kabla ya kitu kingine, huenda ikamwongezea wafuasi wengi zaidi!

 

Kwa upande wa Odinga, maamuzi ya mahakama yanaleta tafsiri ngumu kuwa alishinda uchanguzi huo akachezewa rafu mbaya iliyomwangusha. Hivyo, anaweza kutumia mtaji wa wapiga kura hao waliokumbwa na kadhia ya dhuluma ya kuibwa kwa kura zao, kuwaaminisha tena kuwa yeye ndiye ‘nabii’ atakayewapeleka huko watakako!

 

NA: DAUD MAKOBA| GPL

Leave A Reply