The House of Favourite Newspapers

Bwana Harusi Atoweka Saa Chache Kabla ya Harusi, Bi Harusi Aangua Kilio

0

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Bwana harusi ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la New Hope Mountain (NHM), Yusuph Asagwile Mwakasole mkazi wa Mtaa wa Ilembo Kata ya Iyela, jijini Mbeya ametoroka saa chache kabla ya kufunga ndoa.

 

Tukio hilo limemwacha bibi harusi aitwaye Dorcus Jonas ambaye alitarajia kufunga naye ndoa katika Kanisa la Pentecoste Revival lililopo Iyela Desemba 23, 2020 kwenye wakati mgumu.

 

Akielezea kisa hicho Balozi wa Mtaa wa Ilembo, Alice Mwanangwa alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baba wa bwana harusi Asagwile Mwakasole aliyedai Mchungaji Enock Mgogo wa Kanisa la Pentecoste Revival amegoma kufungisha ndoa hiyo kwa kile alichodai kuwa maharusi walikuwa wamezini kabla ya kufungishwa ndoa.

 

Aidha, ilielezwa kuwa baada ya sintofahamu hiyo ya zuio la ndoa ndipo taarifa za kutoweka kwa bwana harusi zilipojitokeza na kumfanya balozi kutoa taarifa kituo cha Polisi Mwanjelwa kutokana na kuwepo habari za kusadikika kuwa kuna kijana amehusika kumtorosha bwana harusi kumpeleka Dar es Salaam.

 

Inadaiwa kuwa lengo la kijana huyo kumtorosha bwana harusi lilikuwa ni kutafuta sehemu nyingine ya kufunga ndoa ambapo mpango wa kumtorosha bibi harusi nao ulidaiwa kusukwa kimyakimya.

 

Hata hivyo, balozi baada ya kubaini njama hizo alishirikiana na ndugu wa bwana harusi kumkamata kijana huyo (jina linahifadhiwa) ambaye alikiri kuhusika na tukio hilo akidai kutumwa na Askofu wao (hakumtaja jina) aliyeko jijini Dar es Salaam.

 

Kwa upande wake bibi harusi Dorcus alisema hivi karibuni alipigiwa simu na mama askofu wa jijini Dar es Salaam (alikotorokea mchumba wake) aliyedai ameoneshwa katika maono kuwa yeye na mchumba wake Yusuph wameanguka dhambini hivyo wanapaswa kuongozwa sala ya toba kwa kuwa wamezini.

 

Unabii wa mama mchungaji huyo ulipingwa vikali na bibi harusi ambaye alisema “hakuwahi kuzini na mchumba wake huyo hata siku moja.”

Aidha, bibi harusi alisikitishwa na kitendo cha mama askofu kumtuhumu jambo hilo zito.

 

Alisema kuwa licha ya yeye kukataa, mama askofu alimwambia kuwa bwana harusi amekiri kuzini hivyo naye akubali ili aende Dar es Salaam watengeneze na Mungu kabla ya ndoa yao kufungwa.

Dorcus ambaye mara kadhaa alikuwa akiangua kilio, alisema mama askofu wao amemwambia yeye na mchumba wake wanatakiwa kuacha kutoa huduma ya kiroho Mbeya na kuanza maisha mapya jijini Dar es Salaam, jambo ambalo amelikataa.

 

Akisimulia zaidi huku akibubujikwa na machozi, Dorcus alishangazwa na kitendo cha mchumba wake kukata mawasiliano ghafla na kutoroka huku akijua kuwa taratibu zote za ndoa zilikuwa zimekamilika.

“Shela, viatu na nguo za kubadilisha ukumbini siku ya harusi zilikuwa tayari.

 

“Kama aliona kuna kizuizi kanisani ilikuwaje atoroke bila mawasiliano yoyote na anajua maandalizi yote yamekamilika kupitia kamati ya harusi, inauma sana,” alilalamika bibi harusi.

Kwa upande wake mjomba wa bibi harusi na mlezi wake, Sadiki Cornel Mwakihaba alisema kitendo kilichotokea kwa binti yao kimempa fedheha kwani kama familia walipokea michango ya watu na taratibu za kumuaga zilikuwa zimefanyika.

 

Naye baba mzazi wa bwana harusi Asagwile Mwakasole alisema kijana aliyemtorosha mtoto wake ahojiwe vizuri ili aeleze sababu za kufanya hivyo na wapi mwanaye aliko.

 

Naye mchungaji Enock Mgogo wa Kanisa la Pentecoste Revival lililopo Ilembo Kata ya Iyela alisema yeye aliombwa tu kufungisha ndoa ya mchungaji mwenzake Yusuph katika kanisa lake kwa kuwa kanisa la bwana harusi halina kibali cha kufungisha ndoa.

 

“Lakini wakati maandalizi yanaendelea nilipata taarifa kwa askofu wetu kuwa vijana hao wamezini hivyo sipaswi kuwafungisha ndoa, nami nikatii,” alisema mchungaji Mgogo.

Mgogo alisema bibi harusi ni muumini wake na alipomuuliza kuhusu tuhuma za kuzini na mchumba wake alikataa.

Mchungaji Mgogo alisema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika kanisa lake.

 

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya maandalizi ya sherehe, Judith Mgeyekwa alisema kamati ilikamilisha manunuzi ya kila kitu hivyo hawana pesa za kuwarejeshea waliochangia harusi hivyo wanamsubiria bwana harusi arejee ili ndoa ifungwe kama si kanisani basi hata serikalini.

Judith alisikitishwa na kitendo cha mchungaji Mgogo kutotoa taarifa za kusitisha ndoa licha ya kamati kumshirikisha kila jambo katika maandalizi.

STORI: EZEKIEL KAMANGA, MBEYA

Leave A Reply