The House of Favourite Newspapers

Mwinyi Alivyojiuzulu Uwaziri kwa Mauaji ya Kanda ya Ziwa

0

TUNAMALIZA mwaka mpya kwa kuwakumbusha utamaduni ambao husukumwa na maadili ambayo wakubwa serikalini wanaokumbwa na kashfa nzito hulazimika kujiuzulu nyadhifa zao, lakini katika zama hizi maadili haya yametoweka na badala yake wakiharibu husubiri kutumbuliwa.

 

Hata hivyo, si sahihi kabisa kusema kwamba zamani utamaduni wa kujiuzulu kwa wakubwa haukuwapo. Ulikuwapo tangu katika utawala wa Awamu ya Kwanza wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

 

Kwa mfano; Januari 22, 1977 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano, Ali Hassan Mwinyi, alijiuzulu mara moja baada ya kuibuka kwa ripoti za mauaji ya kikatili ya raia katika mikoa ya kanda ya ziwa yaliyofanywa na maofisa usalama chini ya wizara yake.

 

Baadaye Ali Hassan Mwinyi akiwa rais alikuwa kiongozi pekee aliyelifukuza baraza lake lote la mawaziri mapema mwaka wa 1990 baada ya manung’guniko mengi kutoka kwa wananchi kutokana na utendaji mbovu wa majukumu yao. Rais Mwinyi aliwaita Ikulu mawaziri wake wote na kuwaambia anataka wote waandike barua hapo hapo za kujiuzulu nyadhifa zao.

 

Akasimama Joseph Warioba aliyekuwa waziri mkuu na kuuliza: “Hata mimi?” Mwinyi akamjibu: “Naam, hata wewe, kwani Katiba yetu inasema waziri mkuu ni waziri pia.”

 

Akiwa waziri wa mambo ya ndani, Mwinyi aliwahi kuandika barua ya kujiuzulu ikithibitisha jinsi kiongozi huyo alivyo juu kwa viwango vya utiifu na uadilifu.

 

Katika barua hiyo ambayo ilisambazwa kwenye vyombo vya habari kwa sasa, inaonyesha jinsi Mwinyi alivyojiuzulu kwa unyenyekevu hiyo Januari 22, 1977 wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani.

 

Kiongozi huyo ambaye mwaka 1985 alikuja kukwea tena ngazi ya uongozi na kuwa Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika barua aliyomwandikia Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere, alieleza jinsi alivyoguswa na mauaji ya watu wasio na hatia walioshukiwa kuwa wachawi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza mwaka 1975.

 

Kwa maneno yake Mwinyi alisema: “Kisiasa nakiri kuwa nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.”

 

Mwinyi alijikuta katika matatizo hayo baada ya Jeshi la Polisi kuendesha operesheni ya kusaka wauaji wa wachawi katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, na alikiri kwamba:

 

“…vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwemo, vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo viovu vya kishenzi, kinyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika, wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu.”

 

Ingawa Mwinyi aliweka bayana kwa mkuu wa nchi Mwalimu Nyerere, kwamba kijinai asingehusika kwani hakushiriki wala kushauri, kuagiza wala kuelekeza mambo hayo yafanywe hivyo, aliandika barua isiyo na kinyongo kabisa na yenye unyenyekevu mkubwa kwa Rais Nyerere.

 

Kwa unyeyekevu mkubwa, Mwinyi alisema: “Kwa hiyo, Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie kujiuzulu.”

 

Kwa barua hiyo ya Mwinyi ambayo gazeti hili limeamua kunukuu baadhi ya maneno kama ulivyosoma hapo juu kwa nia ya kuamsha uadilifu unaofanana na kiongozi huyo wa awamu ya pili, ni fursa nzuri sasa kwa viongozi wote wa umma kuiga mfano huo ambao humpunguzia rais majukumu ya kutumbua iwapo kuna matatizo mazito yametokea katika ofisi unayoisimamia.

 

Mzee Mwinyi kwa maudhui ya barua yake ya mwaka 1977 haikuwa jambo la ajabu kuja kuwa Rais wa Tanzania miaka minane baadaye, huku akionekana kama kiongozi aliyeshinda vishawishi na kila aina ya hila kwenye uongozi wake.

 

Kupatikana kwa barua hiyo ya Mwinyi ya kujiuzulu na kuwekwa hadharani iliweka mizania mpya kabisa ya uadilifu katika uwajibikaji wa viongozi wa umma wanapoingia matatani na kutakiwa kujiuzulu.

 

Miongoni mwa viongozi wakuu waliowahi kujiuzulu katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, pamoja na mawaziri wawili waliowahi kusimamia Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti za utawala wa awamu hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

 

Viongozi hao, ingawa barua zao za kujiuzulu kwa Rais Jakaya Kikwete hazijapata kuwekwa hadharani, lakini kwa kauli na maelezo yao bungeni wakati wanatangaza kujiuzulu walionyesha kuwa walionewa tu kufikishwa katika hatua hiyo.

 

Kwa mfano, Lowassa alisema wazi “ameonewa na kudhalilishwa sana kisa ni uwaziri mkuu” kuhusiana na suala la mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura ambao ulitolewa kwa kampuni ya Richmond.

 

Baada ya Lowassa na wenzake wawili kujiuzulu kulizuka mpasuko mkubwa miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vita ikapiganwa kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa viongozi hao ulikuwa ni uonevu.

 

Mivutano hiyo ya wabunge ndiyo ilifanya hata Halmashauri Kuu ya CCM kuunda kamati ya wazee watatu wa busara ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi na wajumbe ni Spika wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, kusaka suluhu ya uhasama huo.

 

Wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi ya kusaka suluhu ya uhasama huo, suala la Richmond ambalo ni chimbuko la kujiuzulu kwa viongozi hao watatu, likazidi kuwa tete kila kukicha, zaidi likijitokeza katika makundi ya wapinga ufisadi na wale wanaotajwa kuutetea.

Bila shaka tumejifunza kitu.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, UWAZI

Leave A Reply