The House of Favourite Newspapers

CAF Yatajwa Ujio Kocha Mpya Mfaransa wa Yanga

0

MEFAHAMIKA kuwa Yanga imefikia maamuzi ya kumleta kocha raia wa Ufaransa, Sebastian Migne kwa ajili ya michuano ya Caf ambayo timu hiyo huenda ikashiriki msimu ujao.

Yanga inaamini bado wapo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Pia viongozi wanaamini Tanzania itapeleka timu nne katika msimu ujao, hiyo ndiyo sababu ya kumleta kocha huyo.

 

Migne akitarajiwa kujiunga na Yanga, aliwahi kuifundisha Timu ya Taifa ya Kenya na Equetorial Guinea ambaye atatua kuchukua nafasi ya Mrundi Cedric Kaze.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Migne amepitishwa na Kamati ya Ufundi ya Yanga iliyo chini ya mwenyekiti wake Dominic Albinius kutokana na uzoefu alionao wa michuano ya kimataifa.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kingine kilichowavutia ni uzoefu wake wa kulijua vizuri soka la Afrika, hivyo wana matumaini makubwa naye katika kufikisha malengo yao katika msimu ujao.

 

Aliongeza kuwa kocha wakati wowote kuanzia wiki hii atatua nchini tayari kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili, lakini atakabidhiwa mikoba ya ukocha mkuu baada ya msimu huku akiwa na jukumu la kuifuatilia timu na kutoa ushauri kabla ya muda huo kufika.

 

“Kama unavyofahamu msimu ujao tuna nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa, hata kama tusipokuwa mabingwa na hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa timu nne Tanzania.

 

“Hivyo ni lazima tuliboreshe haraka benchi letu kwa kuanzia na baada ya hapo tutakwenda katika usajili na jukumu hilo tumempa kocha huyo Migne ambaye atasimamia zoezi zima katika kuijenga timu imara ya ushindani wa kimataifa.

 

“Kama uongozi tunaamini uwezo na uzoefu mkubwa alionao Migne katika ushiriki wetu wa michuano ya kimataifa mwakani na zaidi analijua vema soka la Afrika na hiyo ni kutokana na kuwahi kufundisha timu ya taifa ya Kenya,” alisema mtoa taarifa huyo.Akizungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassan Bumbuli, alisema:

 

“Hilo suala la kocha bado lipo kwenye Kamati ya Utendaji ya Yanga na kama likikamilika basi haraka tutatoa taarifa kwenye vyombo vya habari.“Mchakato huo wa kumpata kocha mpya unakwenda vizuri, kwani Kamati ya Utendaji ya Yanga imepitia CV 72 za makocha mbalimbali lakini baada ya mchujo yalibaki majina matatu, hivyo Wanayanga wanatakiwa kuwa watulivu katika kipindi hiki.”

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply