The House of Favourite Newspapers

CAG ASEMA AMETIMIZA WAJIBU WAKE, UAMUZI WA BUNGE NI WAO

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad,  amesema amekwishatimiza wajibu wake na kwamba uamuzi wa bunge wa kususa kushirikiana naye si shughuli yake.

 

Prof. Assad ameyasema hayo leo katika mahojiano kwenye kipindi cha Jambo kilichorushwa asubuhi hii na shirika la habari la utangazaji la TBC.

 

Amesema uamuzi wa bunge ni uamuzi wa bunge, na kwamba ofisi yake ya CAG ni ofisi huru, akiwa amekamilisha kazi yake kwa mwaka huu na kuikabidhi ripoti ya ukaguzi kwa Rais John Magufuli, na kinachofuata ni mchakato wa bunge, si kwa upande wake tena.

 

Kuhusu bunge kukataa kushirikiana naye, amesema ameusikia uamuzi huo na hajaufanyia tathmini, na amelitaka bunge liweke wazi  kumbukumbu ya matamko na shughuli za bungeni (Hansard) kuhusu kuhojiwa kwake ili Watanzania wajue aliulizwa nini na alijibu nini.

 

“Majukumu ya CAG yameainishwa na katiba na inataka nifanye kazi na bunge,” alisema Assad na kuongeza kwamba uamuzi huo unaweza kuleta mgogoro wa kikatiba kwa sababu tayari ripoti ameishaiwasilisha kwa rais kwa mujibu wa katiba, na ripoti hiyo lazima iwasilishwe bungeni ndani ya siku saba,” alisema na kuongeza kwamba ripoti hiyo isipowasilishwa bungeni utakuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Comments are closed.