Carlinhos ni Balaa Kubwa Yanga SC

BAADA ya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Carlos Carlinhos, juzi Jumamosi kuifungia Yanga bao la ushindi dhidi Mtibwa Sugar, sasa mchezaji huyo anakuwa kafikisha uchangiaji wa mabao matano katika michezo 6 pekee aliyoicheza Yanga katika ligi kuu msimu huu.

 

 

Mchezaji huyo tangu asajiliwe na Yanga katika dirisha kubwa, ameshindwa kucheza michezo mingi kutokana na majeraha ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakimsumbua.

 

 

Carlinhos aliifungia Yanga bao katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa katika mchezo uliofanyika juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, akipokea pasi kutoka kwa Tuisila Kisinda.

 

 

Katika mchezo huo Carlinhos aliingia katika dakika ya 70 akichukua nafasi ya Ditram Nchimbi ambapo ilimchukua dakika 2 tu mchezaji huyo kuifungia Yanga bao ambalo lilidumu mpaka mpira unamalizika.

 

 

Sasa kiungo huyo anakuwa amefikisha mabao matatu na asisti mbili katika michezo sita ya ligi kuu ambayo ameichezea klabu hiyo tangu asajiliwe katika dirisha kubwa la usajili.

 

 

Aidha, pasi mbili za mabao za Carlinhos alizozitoa ilikuwa katika michezo dhidi ya Mbeya City katika ushindi wa Yanga wa bao 1-0 akitoa asisti kwa Lamine Moro, pasi nyingine ilikuwa katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini akitoa pasi kwa Lamine Moro.

 

 

Katika upande wa mabao kiungo huyo alifunga katika mchezo dhidi ya Coastal Union Yanga ikishinda mabao 3-1, dhidi ya Namungo katika sare ya bao 1-1 na katika mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa, Yanga ikishinda kwa bao 1-0.

 

 

Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa mchezaji huyo amekuwa hatari zaidi pindi anapopewa nafasi ya kucheza kwani katika michezo sita aliyocheza, amechangia idadi ya mabao matano.

 

 

Marco Mzumbe,

Dar es Salaam

Toa comment