The House of Favourite Newspapers

Chalamila Awatimua Wanafunzi Waliochoma Shule

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila,  amewafukuza shule wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya ambao pia wanakabiliwa na kesi mahakamani ya kuchoma mabweni mawili ya shule.

Ametoa maamuzi hayo leo Jumatano, Oktoba 23, 2019, akiwa shuleni hapo wakati akitoa ripoti kuhusiana na tukio la kuwasimamisha shule wanafunzi waliohusika kuchoma mabweni shuleni hapo ambapo wote  walitakiwa walipe faini ya Shilingi 200,000/= kwa kila mmoja, na faini ya Shilingi 5000,000 kwa kila aliyechoma moto mabweni hayo.

Wanafunzi hao  waliofukuzwa watafunguliwa mashtaka mahakamani na hawataruhusiwa kufanya mtihani wa taifa kwa miaka mitano.

“Nimewatimua wanafunzi wote ambao hawajalipa faini na nitaandika ripoti kwenye mamlaka husika kuwazuia wasifanye mitihani tena kwa muda wa miaka mitano, na kama kuna shule yoyote itawapokea itakuwa hatarini.

“Jinsi ya kuwafuatilia hawa wanafunzi ni ndogo sana, kwa sababu tunawafahamu tangu walipoanzia mpaka wapo sasa na uzuri zaidi tumewalipia ada wenyewe wala hawatusumbui kuwapata,” amesema.

Mapema mwezi huu aliwaadhibu wanafunzi hao kwa kuwacharaza bakora na kisha kuwasimamisha masomo wanafunzi wote waliohusika kwenye vurugu na kuchoma mabweni hayo na kuwataka wakirudi shuleni hapo warudi na faini kwa ajili ya ukarabati wa mabweni.

 

Comments are closed.