The House of Favourite Newspapers

Chama Agomea Mkataba Simba, Arudi Zambia

0

KIMENUKA! Ndivyo utakavyoweza kusema, ni baada ya kiungo mchezeshaji fundi wa Simba, Mzambia, Clatous Chama, kugoma kuongeza mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo.

 

Hiyo ni siku chache tangu uongozi wa timu hiyo ufanye mazungumzo na staa huyo anayetarajia kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

 

Kiungo huyo ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu, mwingine ni Hassani Dilunga, Yusuph Mlipili, Mohamed Ibrahim na Paul Bukaba.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kiungo huyo hivi sasa yupo nyumbani kwao alipokwenda kwenye mapumziko ili kupisha ugonjwa wa Corona ligi ikiwa imesimama.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo alifuatwa na viongozi wa Simba kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo huku akiomba muda zaidi kujifikiria kabla ya kusaini mkataba huo.

 

Aliongeza kuwa, kiungo huyo ameomba kuanza mazungumzo ya kusaini mkataba huo mara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu, kitu ambacho viongozi hawataki wakihofia kuzidiwa ujanja na klabu nyingine.

 

“Upo uwezekano mkubwa wa Chama kuihama Simba mwishoni mwa msimu huu wa ligi, hiyo ni baada ya kugomea mkataba mpya aliopewa kwa ajili ya kusaini baada ya ule wa miaka miwili kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

“Hivyo, Chama ameomba kusaini mkataba huo baada ya ligi kumalizika, kitu ambacho viongozi hawataki kusikia kwa hofu ya nyota huyo kutimka wakati bado kocha anaonekana kumuhitaji.

“Inasemekana Chama hana furaha katika timu hiyo kutokana na viongozi kuingilia uhuru wa maisha yao binafsi nje ya soka,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Dk Arnold Kashembe kuzungumzia hilo alisema: “Hilo suala ni la kiutawala, hivyo siwezi kulizungumzia kwa hivi sasa na muda wa usajili bado.”

 WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply