DIRISHA la usajili wa Ulaya lilifungwa tangu Agosti 31, mwaka huu, kabla ya kufungwa usajili uliowashangaza wengi ni Liverpool kumsajili kiungo mshambuliaji Oxlade-Chamberlain kutoka Arsenal.
Alisajiliwa kwa ada ya pauni milioni 35, lilionekana ni dau kubwa huku sababu hasa ya kuhama kwa mchezaji huyo ni kama haikuwaingia watu wengi akilini.
Moja ya sababu iliyosababisha mchezaji huyo kuondoka Arsenal ni kitendo cha kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger kumtumia katika nafasi ya kushambulia akitokea pembeni wakati yeye anataka kucheza katikati.
Kingine ambacho kilionekana kuwa kimechangia uhamisho wake ni kitendo cha Arsenal kukosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) huku Liverpool ikipata nafasi hiyo.
Kabla ya uhamisho wake huo, Arsenal ilikutana na kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Liverpool katika Premier League, kipigo hicho inawezekana kilinogesha maamuzi ya Chamberlain kuamini kuwa Liverpool ni sehemu sahihi kwake.
Kabla ya Arsenal kupata kipigo kutoka kwa Liverpool pia ilikuwa imetoka kupokea dozi kutoka kwa Stoke City, hivyo ikaonekana kama Arsenal inapoteza dira mapema tu mwa msimu huu wa 2017/18.
Baada ya Chamberlain kuchukua maamuzi ya kuhama Arsenal, inavyoonekana ni kama kibao kimegeuka, kwani tangu atue Liverpool hali ya mambo bado imekuwa mbaya kwa mchezaji huyo na kwa timu yake kwa jumla.
Tangu Chamberlain atue Liverpool timu hiyo haijapata ushindi wowote wakati ambapo Arsenal wao hawajapoteza mchezo wowote tangu kuondoka kwake.
Kipigo ambacho Liverpool imekipata cha mabao 2-0 kutoka kwa Leicester na kuiondoa timu hiyo katika michuano ya Carabao Cup, Jumanne iliyopita kimeendelea kumpa presha kubwa mchezaji huyo ambaye alicheza mechi yake ya kwanza kwa dakika 90 akiwa ndani ya jezi ya Liverpool.
Licha ya Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kufanya mabadiliko ya kikosi katika mchezo huo, bado lawama nyingi zinaonekana kumuangukia Chamberlain ambaye hajaonyesha makali tangu ameanza kupewa nafasi.
Katika mchezo huo Chamberlain alipangwa kucheza nafasi ya kushambulia akitokea pembeni na siyo katikati kama ambavyo amekuwa akitaka, lakini kutokana na kiwango anachokionyesha baadhi ya mashabiki wao w a m e a n z a kuhisi kuwa mchezaji huyo ana ‘gundu’ na kuanza kumlaumu.
U p a n d e mwingine ni kuwa mashabiki wa Arsenal nao wameanza kuwadhihaki wale wa Liverpool wakiwaambia kuwa wamebeba mzigo ambao wao uliwashinda.
M c h e z o wake wa kwanza akiwa Liverpool licha ya kuanzia b e n c h i , Chamberlain alishuhudia timu yake ikipata kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Manchester City, baadaye ikafuata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sevilla katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya hapo Liverpool ikapata sare ya bao 1-1 dhidi ya Burnley katika Premier League.
Utani ambao umekuwa ukitawala kwenye mitandao ya jamii na mingine ya michezo ni juu ya kiwango cha Chamberlain ambapo thamani iliyotumika kumsajili na kile kinachoonekana uwanjani vinaonekana kuwa ni vitu viwili tofauti.
Kingine ni kuwa katika mchezo ujao wa wikiendi hii wa Liverpool ni kuwa wanatarajiwa kukutana na wapinzani wao haohao, Leicester City lakini safari hii ni katika Premier League, hivyo Liverpool italazimika kufanya kazi ya ziada kuwaaminisha mashabiki wao k u w a tatizo siyo Chamberlain.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakisema kuwa mchezaji huyo ana laana ya Wenger kwa kuwa ni kocha ambaye alichangia kumsimamia tangu alipomsajili akiwa chipukizi akitokea Southampton.
Wenger alimvumilia licha ya kuwa hakuwa katika ubora wa juu kama ilivyotegemewa lakini baada ya kuona mambo hayaendi vizuri na timu hiyo inapitisha miaka mingi bila kutwaa ubingwa wa Premier ameamua kuondoka
Mashabiki wengine wa Arsenal wamesema kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hana uwezo wa kutosha, hivyo kusajiliwa na Liverpool ni sawa na kuwapunguzia mzigo wao.
Shabiki mwingine akawazodoa kwa kusema kuwa Liverpool walikataa pauni milioni 100 za kumuuza Coutinho kisha wakamsajili Chamberlain kwa pauni milioni 35 kitu ambacho ni kibaya kibiashara.
Hivyo, Liverpool inahitaji ushindi katika wikiendi hii, kinyume na hapo presha itaendelea kuwa kubwa kwa Chamberlain ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya England.