The House of Favourite Newspapers

Charles Quansah; Muuaji Hatari Zaidi Kuwahi Kutokea Nchini Ghana

0

-Alikuwa akiwabaka kisha kuwaua kwa kuwanyonga au kuwachinja wanawake

-Alikuja kukamatwa baada ya kuchomwa na mpenzi wake aliyewapigia simu polisi

– Kwa kinywa chake akakiri kuwaua wanawake tisa huku akihusishwa na mauaji ya wanawake wengine 34.

 

Charles Kwabena Ebo Quansah, ni jina linaloogopwa sana hususani na wanawake katika mitaa ya Jiji la Accra na Kumasi nchini Ghana!

 

Japokuwa kwa sasa bado anaendelea kusubiri kutekelezwa kwa hukumu yake ya kifo katika Gereza la Nsawam Medium Security Prison jijini Accra, bado wanawake wengi hawaamini kama yupo gerezani, wanahisi wanaweza kukutana naye mitaani na akawatendea ukatili wa kutisha, kama aliowahi kuutenda kwa wanawake tisa waliopoteza maisha kwenye mikono yake.

 

Mwishoni mwa miaka ya 1990, wimbi kubwa na la kutisha lilizuka nchini Ghana hususan katika Jiji la Accra na Kumasi, ambapo wanawake walikuwa wakibakwa na kuuawa kikatili na watu wasiojulikana.

 

Mazingira ya mauaji yalikuwa yakifanana, wote walikuwa wakifanyiwa ukatili huo kisha kunyongwa, ushahidi wa kimazingira ukaonesha kwamba aliyekuwa akifanya matukio hayo, alikuwa ni mtu mmoja kutokana na jinsi mfanano wa matukio hayo ulivyokuwa.

 

Mfumo wa muuaji ilikuwa ni kumuwekea mtego mwanamke anayemtaka, kisha kumteka na kumpeleka mafichoni! Huko angembaka kisha baada ya kumaliza haja za mwili wake, angemuua kwa kumnyonga shingo au kumchomachoma na visu mpaka mtu apoteze maisha.

 

Hali ikazidi kuwa mbaya mwaka 1998 na 1999 ambapo takribani wanawake thelathini, walipoteza maisha katika matukio yanayofanana. Vyombo vya ulinzi na usalama vikawa vinatumia kila mbinu kuhakikisha vinampata muuaji haraka iwezekanavyo, kabla hajasababisha mauaji mengine.

 

Hata hivyo, haikuwa rahisi, muuaji aliendelea kudunda mitaani! Siku moja, ndipo msichana mmoja alipopiga simu polisi. Ilikuwa ni majira ya usiku, akawaambia askari kwamba, kuna jambo lisilo la kawaida, limetokea kwa mpenzi wake.

 

Akaeleza kwamba, alikuwa amerejea nyumbani huku nguo zake zikiwa na damu, na alipomuuliza, alimweleza kwamba alikuwa amevamiwa na vibaka, ajabu ni kwamba hakuwa na jeraha lolote kwenye mwili wake.

 

Ni hapo ndipo polisi walipoacha kila walichokuwa wanakifanya na kuelekea eneo la tukio, hatimaye wakafanikiwa kumkamata mwanaume aitwaye Charles Kwabena Ebo Quansah.

 

Ajabu zaidi ikawa ni kwamba, mwanaume huyu alikuwa akiendelea kuchunguzwa na polisi kutokana na mauaji ya mwanamke mwingine aliyekuwa na uhusiano naye wa kimapenzi, Joyce Boateng.

 

Mpaka hapo, polisi wakawa wameshapata pa kuanzia, Charles Quansah akawa ndiye mshukiwa wa kwanza wa mauaji yaliyokuwa yanaendelea nchini humo. Hiyo ilikuwa ni Februari, 2000.

 

Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, ikaja kubainika kwamba ndiye aliyeshiriki pia kwenye mauaji ya mwanamke mwingine, Akua Serwaa ambaye alikutwa akiwa amenyongwa hadi kufa jirani na Uwanja wa Mpira wa Kumasi, tukio lililotokea Januari 19, 1996. Msichana huyo alikuwa akifanya kazi saluni katika Mji wa Kumasi na kabla ya kunyongwa, alikuwa amebakwa.

 

Inaelezwa kwamba, akiwa kwenye mikono ya polisi, alibanwa kisawasawa, akaendelea kutoa ushuhuda wa matukio yote aliyoyafanya, akakiri kwamba tayari alikuwa amewaua wanawake tisa kwa mikono yake baada ya kuwabaka.

 

Polisi hawakuishia hapo, wakaendelea na uchunguzi na baadaye, wakaja kubaini kwamba, Quansah, hakuwa ameshiriki kwenye mauaji ya wanawake tisa pekee, bali zaidi ya wanawake 34! Yule muuaji aliyekuwa anatafutwa, ndiye huyu aliyekuwa kwenye mikono ya polisi kwa wakati huo.

 

Mwanaume huyu alizaliwa mwaka 1964 na kupewa jina la Charles Kwabena Ebo Quansah kama ilivyoelezwa na vitendo vyake vya ukatili na mauaji, vikamfanya apachikwe jina jingine la The Accra Strangler, Mnyongaji wa Accra.

 

Quansah alikuwa akifanya kazi ya ufundi makenika na inaelezwa kwamba kabla ya kuhamia jijini Accra, alikuwa akiishi katika mji mdogo wa Adenta.

 

Historia ya matukio yake ya uhalifu, ikiwemo wizi, kubaka na mauaji, inaanzia mwaka 1986. Kwa mara ya kwanza, alikamatwa na kufungwa katika Gereza la James Fort, baada ya kukutwa na hatia ya kubaka, hiyo ilikuwa ni mwaka 1986.

 

Baadaye aliachiwa na kurudi uraiani ambapo mwaka mmoja baadaye, 1987, alikamatwa tena kwa tuhuma za kubaka, akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela ambayo aliitumikia katika Gereza la Nsawam Medium Prisons lililopo nje kidogo ya Jiji la Accra.

 

Baada ya kumaliza hukumu yake, alirejea tena uraiani ambapo kwa mara nyingine, mwaka 1996 alikamatwa kwa wizi, akahukumiwa na kurudishwa kwenye Gereza la Nsawam Medium Prisons.

 

Baada ya kumaliza hukumu yake, ni hapo ndipo alipoamua kuyahama makazi yake ya awali na kuelekea katika Jiji la Accra, ambalo ndiyo mji mkuu wa Ghana. Kesi ya mauaji ya mpenzi wake, ilianza kusikilizwa Alhamisi ya Julai 11, 2002 katika Mahakama Kuu ya Accra.

 

Kesi iliendelea kunguruma na sijui ni nini kilichotokea, lakini kesi iliyokuja kusababisha ahukumiwe kunyongwa hadi kufa, ilikuwa ni ile ya kumbaka kisha kumuua Akua Serwaa kisha kumtupa jitani na Uwanja wa Mpira wa Kumasi, tukio lililotokea Januari 19, 1996.

 

Baada ya kuhukumiwa, akiwa gerezani akiendelea kusubiri kutekelezwa kwa adhabu yake, mwaka 2003 Quansah alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kwamba, siyo kweli kwamba alifanya vitendo hivyo bali mateso makali aliyokuwa akipewa na polisi wakati wa upelelezi wa kesi hiyo, ndiyo yaliyomfanya akiri makosa ambayo hakuwahi kuyafanya.

 

Mpaka makala haya yanaandaliwa, mwanaume huyo anasubiri kutekelezwa kwa hukumu ya kunyongwa hadi kufa! Huyo ndiyo Charles Kwabena Ebo Quansah, muuaji aliyeitingisha Ghana!

 

Leave A Reply