The House of Favourite Newspapers

Chirwa, Sure Boy Kuwekwa Karantini Azam

0

UONGOZI wa Azam umesema kuwa unatarajia kuwaweka wachezaji wake karantini ya siku 14 wakiwemo kiungo mshambuliaji, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji, Mzambia, Obrey Chirwa kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kujikinga na Virusi vya Corona.

Uongozi huo umetoa kauli ikiwa ni baada ya ligi kusimama kutokana na janga hilo huku baadhi ya wachezaji wa kimataifa wakiwa wamerejea katika mataifa yao wakiwemo, Wazimbabwe, Donald Ngoma, Bruce Kangwa, Never Tigere, Razak Abalora , Daniel Amoah na Yakubu Mohammed raia wa Ghana pamoja na Mganda, Nicolaus Wadada.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya timu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’, alisema kuwa wamepanga kuchukua uamuzi wa kuwaweka wachezaji wote karantini kwa kuwa watakuwa wanatoka katika maeneo yenye mikusanyiko iliyokuwa inawakutanisha na watu wengine.

 

“Kwanza waliopo nje wakirejea lazima wafuate utaratibu ambao umewekwa na Serikali wa kukaa karantini ya siku 14, halafu wakishakuja kwetu watakaa na wachezaji wa hapa ambao nao kwa sasa wamerejea katika familia zao kwa muda wa siku 14 katika uangalizi maalumu kutokana na ukubwa wa hili janga la Corona.

 

“Lengo kubwa la kufanya hivyo ni kutaka kujiridhisha juu ya wachezaji wetu kuhusu afya zao kwa sababu hata wachezaji wa ndani bado wanakutana na watu wengi huko kwenye familia zao sasa uongozi lazima tufanye kitu ambacho kitakuwa na faida kwa kila mmoja wetu kabla ya kuanza rasmi mazoezi pale hali itakapokuwa imetengemaa,” alisema Zakaria

Stori: Abdulghafal Ally na Ibrahim Mussa

Leave A Reply