The House of Favourite Newspapers

Chondechonde; Baada ya Sikukuu Kuna Januari

0

MSIMU wa sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya mara nyingi hazituachi salama mifukoni. Katika kipindi hiki tunapokuwa mapumziko na familia zetu ni muda muafaka wa kujitathmini na kuweka mambo sawa kwa ajili ya kuanza mwaka 2020.

 

Pamoja na hayo, kipindi hiki huusisha manunuzi makubwa ya bidhaa na huongeza matumizi ya pesa katika ngazi ya familia. Lakini kwa wafanyabiashara ni kicheko kwa sababu mauzo na faida huongezeka.

 

Sikukuu hizi zinaweza kuwa na furaha, lakini zikatuachia maumivu mwezi Januari.

Ili kujiepusha na maumivu baada ya sikukuu hizi za mwisho wa mwaka, jaribu mambo haya ili kuhakikisha manunuzi yako yanaendana na hali yako ya kipesa.

 

BAJETI…BAJETI!

Ni vema kutengeneza bajeti ya vitu utakavyonunua kabla ya kwenda dukani ili kujiweka katika nafasi ya kutokutumia kiasi kikubwa cha pesa bila kutarajia.

Hii inatokana na ukweli kwamba, maduka mengi yana bidhaa nyingi za kuvutia ambapo usipokuwa makini, utajikuta unataka kununua kila kitu ili kutimiza furaha yako.

 

Jipange kabla ya kufanya manunuzi na dhibiti tamaa ya kuzidisha manunuzi.

Manunuzi ya bidhaa mtandaoni yatakusaidia kupunguza kidogo gharama za usafiri na muda utakaotumia kutembelea maduka mbalimbali katika eneo lako. Pia itakuepusha na msongamano wa watu na magari yanayokwenda kwenye maduka makubwa.

 

Njia hii ni nzuri kwa sababu mnunuzi anakuwa na uchaguzi mpana wa bei za bidhaa zinaonekana mtandaoni na akikamilisha oda yake, bidhaa inamfikia alipo.

Pia unaweza kutumia program ya kufuatilia na kulinganisha bei za maduka mbalimbali ili kufanya uamuzi sahihi na kupata punguzo la bei.

 

Njia hii ni nzuri kwa sababu mnunuzi anakuwa na uchaguzi mpana wa bei za bidhaa zinaonekana mtandaoni na akikamilisha oda yake, bidhaa inamfikia alipo. Nunua bidhaa inayodumu muda mrefu. Unaweza kununua bidhaa ambayo itatumika hata baada ya msimu wa sikukuu kuisha ili kupunguza gharama za kununua bidhaa ya aina moja mara kwa mara.

 

Sambamba na hilo, nunua bidhaa ambayo inapendwa na familia yako ili kujenga kumbukumbu inayoweza kusaidia kuimarisha upendo na uhusiano wenu.

Hata hivyo, usiogope kununua bidhaa nyingi za aina moja hasa kama ni zawadi ambazo unataka kuwapa watu wengi, kwa sababu maduka yanatoa ofa mbalimbali.

 

Fanya manunuzi kwenye maduka makubwa. Kama umeshindwa kufanya manunuzi mtandaoni, unaweza kwenda katika maduka makubwa ambayo hutoa huduma mbalimbali kama migahawa, burudani, kumbi za starehe na maegesho ya magari yasiyotoza pesa nyingi.

 

Hii itakurahisishia kama mmetoka familia yote kwenda katika manunuzi na kukusaidia kupunguza gharama za kutembelea maeneo tofautitofauti.

Kwa wakazi wa Dar unaweza kwenda kwenye maduka kama Mlimani City, City Mall na mengine ambayo yanakupa wigo mpana wa kupata huduma nyingi kwa wakati mmoja.

 

Siku za mwisho wa wiki, maduka mengi huwa na msongamano mkubwa wa watu, kama hupendi kashikashi basi kamilisha manunuzi yako siku za kawaida hasa nyakati za jioni.

Nenda dukani peke yako licha kuwa haifurahishi ukilinganisha kama uko na marafiki au familia. Hii itakusaidia kuokoa muda na kukuepusha na ushawishi wa kutumia pesa nyingi kwa mambo yasiyo ya lazima.

 

Jambo lingine unalotakiwa kuwa makini nalo wakati wa sikukuu ni namna sahihi ya kufanya miamala bila kuvuruga bajeti yako.

Kila mtu ana akaunti yake ya benki au simu anayoitumia kutunza pesa. Kama bado hautumii mtandao kufanya malipo, ni muhimu kufanya miamala mapema kuliko kusubiri mpaka siku ya manunuzi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

 

Hii itakusaidia pia kujua kiasi cha pesa ulichonacho na kama bajeti haitoshi utatafuta namna ya kuweka sawa.

Hata hivyo, mapumziko ya mwisho wa mwaka ni kipindi cha kushusha pumzi, kujumuika na marafiki, familia na ndugu ili kuepuka shughuli zinazoweza kukuletea msongo.

Panga mambo yako vizuri, fanya manunuzi kulingana na uwezo wako. Kumbuka kuna maisha baada ya sikukuu hasa mwezi Januari ambao mtu hukabiliwa na mambo mengi yanayohitaji pesa.

Nakutakia Heri ya Krismasi na Mwaka Mpya 2020!

Leave A Reply