The House of Favourite Newspapers

Chongolo Ahimiza UVCCM Kutimiza Wajibu Wake, Kukitangaza Chama kwa Wananchi

0
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo akizungumza
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Daniel Chongolo amewataka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kutambua na kutimiza wajibu mkubwa walionao kwa chama hicho, hasa katika kukilinda na kukisemea ili kizidi kuwa imara na kizidi kuaminiwa kubeba dhamana ya kutawala na kuongoza nchi.
Ndugu Chongolo amesisitiza pia kuwa Chama Cha Mapinduzi kinawategemea vijana hao wa UVCCM kutumia nafasi zao, kubeba agenda za Chama zenye maslahi kwa taifa na Watanzania, na kamwe wasikubali kuhusishwa kuwa sehemu ya kubeba maslahi binafsi ya watu wachache, wenye ndoto zinazokinzana na misingi ya Chama.
Katibu Mkuu Chongolo ameyasema hayo leo Jumanne, Juni 27, 2023, alipokuwa akihutubia Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, waliokutana katika kikao chao cha kawaida, kwenye Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Taifa, jijini Dodoma.
“Chama chetu…Chama Cha Mapinduzi kinawategemea sana Jumuiya ya Umoja wa Vijana Tanzania. Kinawategemea kukilinda na kukisemea na kufanya mambo yakayokifanya kiendelee kuwa chama tawala nchini na si vinginevyo. Tusiache wajibu huo. Tusiache kulinda viongozi wetu. Tusibebe jukumu la kuwa viongozi wa watu. Narudia kwa kusisitiza. Tuwe viongozi wa jumuiya.”
“Hasara ya kuwa kiongozi wa mtu…ni hasara unayojitengenezea kuwa daraja la kukuharibia kesho yako. Ukiwa kiongozi unayesimama na kujitegemea, utaishi miaka yote ukiwa unaendelea kufaidi fursa ya uongozi uliojitengenezea mwenyewe. Lakini ukiamua kuwa kiongozi mfuasi wa mtu, yule mtu akiondoka, na wewe unakwenda na maji. Na mara nyingi watu tunaowafuasia ni watu wenye ndoto,” amesema Ndugu Chongolo na kuongeza;
“Kuna watu maisha yao ni ndoto na ni ndoto kweli kweli. Acheni na achaneni na ndoto za watu. Ishini na ndoto za uhakika, ndoto za taasisi…ndoto za CCM. Simameni na viongozi halali na sahihi wa taasisi na sio viongozi wanaojiandaa kuwa viongozi bila kuandaliwa na taasisi. Viongozi wengi wanaojiandaa na kuwa na tamaa ya nafasi, kwenye chama hiki huwa hawapati nafasi. Nendeni kwenye historia. Sasa ninyi msiwe wafuasi wa wanaojiandaa. Kuweni wafuasi wa taasisi.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Ndugu Mohamed Ali Mohamed Kawaida, ametoa wito kwa wajumbe wa kikao hicho, ambao ni pamoja na Wenyeviti wa UVCCM Mikoa, Makatibu wa UVCCM Mikoa na Wajumbe wa Baraza kutoka mikoa yote ya Kichama, Tanzania Bara na Zanzibar, kuhakikisha wanaketi na kusimamia vikao vya ngazi zao hadi chini na kufanya ziara za kuimarisha jumuiya hiyo katika ngazi zote.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Ndugu Mohamed Ali Mohamed Kawaida
“Nitoe wito na kwenu na ninyi mnavyo vikao vyenu kule chini, kwa Wenyeviti, Makatibu pamoja na Wajumbe wa Baraza Kuu. Niwaombeni sana mkasimamie vikao hivyo, viendelee na vifanyike. Kwa sababu kwenye vikao ndipo tunapotoka na maazimio sote ya pamoja, kauli ya pamoja na uelewa wa pamoja.”
“Lakini sambamba na hilo, niwekee mkazo katika suala zima la ziara. Niwapongeze baadhi ya maeneo, nimekuwa nikiwafuatilieni kwa karibu. Mmekuwa mkifanya ziara katika maeneo yenu. Niwaombe kwa wale bado. Ziara hizo zikaanze au zikaendelee. Na zira hizo zikianza ama zikiendelea, basi zisiwe ziara za kupiga picha bali ziwe ziara za kuleta tija katika chama chetu na kwa Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi,” amesema Ndugu Kawaida.
Leave A Reply