CHUNUSI ZINAVYOHARIBU USO NA UHUSIANO NA TENDO LA NDOA

KUMEKUwepo na imani kwamba suluhisho la tatizo la chunusi ni kushiriki ngono. Katika makala haya leo tutaona kwa undani juu ya tatizo hili na tutaona ukweli wa kutatua ugonjwa huu wa ngozi.   Chunusi au ‘acne’ au ‘pimples’ kama zinavyojulikana, huathiri ngozi ya uso na sehemu nyingine za mwili na kuharibu mwonekano wa mtu kwa kumwachia alama au makovu.

Chunusi hutokea baada ya vifuko vya ngozi vinavyohifadhi mafuta ‘skin oil glands’ kutengeneza ute mafuta mwingi uitwao ‘sebum’ ambao ndiyo husababisha kuziba huko. Chunusi pia husababishwa na maambukizi ya bakteria waitwao ‘propioni bakteriaum acnea’ ambao huishi kwenye ngozi na husubiri kujipenyeza  kwenye vifuko hivyo. Chunusi hujitokeza zaidi usoni, shingoni, mgongoni, kifuani na mabegani. Chunusi ni ugonjwa wa ngozi unaojitokeza sana ingawa siyo ugonjwa wa kutisha, tatizo ni kumwachia mtu makovu ya kudumu mwilini.

CHUNUSI ZINAVYoATHIRI NGoZI

Tatizo hili huwatokea zaidi vijana wa kiume na wa kike. Wanaume huwa hawasumbuliwi sana kama wanawake. Tatizo hutokea kwa njia tofauti kwa kila mmoja. Wanaume huwa hawasumbuliwi sana, lakini ikitokea huwa mbaya sana kama majipu, lakini wengi huwatokea kwa kiasi kidogo. Kwa upande wa wanawake, tatizo hili linahusishwa na mabadiliko katika mfumo wa homoni ambapo zaidi inahusisha katika kipindi cha hedhi na ujauzito.

Kwa mwanamke, tatizo hili huwa linatokea halijalishi usichana hata ukiwa mtu mzima chunusi zinaweza kukutokea. Mwanamke pia unaweza usiwe na historia ya  kuwa na chunusi nyingi  au mbaya katika maisha yako na kujikuta unazipata kwa mara ya kwanza katika umri wa miaka30 au 40. Kwa wanawake wengi, chunusi ni tatizo linalowaweka katika wakati mgumu kwani linawabadilisha  muonekano na kuvuruga urembo halafu hawajisikii vizuri mbele za watu.

AINA ZA CHUNUSI

Zipo aina nne za chunusi zinazoharibu ngozi ya uso. Kwanza ni chunusi ndogo nyeusi ambazo hutokea mojamoja usoni, hasa upande wa mashavu na paji la uso. Chunusi hizi huuma zikiguswa na ukizitumbua hutoa vitu vyeupe, majimaji na damu kidogo. Hii ni kutokana na uchafu wa jasho usoni na mafuta unayopaka usoni ambayo siyo mazuri kwako, zinaitwa ‘comedo’. Aina ya pili ya chunusi ni zile kubwa kiasi zinazojitokeza kwa

mbali na huwa mojamoja, kwa juu inaweza isichomoze, lakini kwa chini huvimba na kuwa nene na pembeni nyekundu. Chunusi hizi huvimba kama majipu na zinauma sana, zikipasuliwa hutoa usaha kiasi, kidonda chake kikipona huacha kovu kama doa jeusi kwenye ngozi.

Zinaitwa Pustules au Pimples. Aina ya tatu ni chunusi ambazo ni mbaya sana na ni hatari kwani husababisha kidonda kwenye ngozi, zina maumivu makali, huwa kama vijipu uchungu, hazipasuki kutoa usaha mwingi bali hutoa tu mdomo na usaha kidogo sana, hufanya vinundunundu usoni na vikipona huacha makovu makubwamakubwa usoni.  Aina hii ya chunusi huitwa Nodules.

Aina ya mwisho ni chunusi vinundu, ni kama hiyo iliyopita, lakini hii inajitokeza kama uvimbe kwa juu ya ngozi, uvimbe huu una maumivu makali na ikiminywa hutoa majimaji na usaha mwingi kuanzia chini kabisa na kujitokeza juu kama jipu. Aina hii ya chunusi huwa haziwi nyingi, hutokea mojamoja, inaweza kutokea kwenye paji la uso, mashavuni pembeni au kwa mbele au hata kidevuni. Ikipasuka huacha kovu kubwa. Wakati mwingine huweza kusababisha homa.

NINI KINASABABISHA CHUNUSI?

Zipo sababu saba za chunusi kutokea. Mabadiliko ya vichocheo au homoni wakati wa balehe. Hii huwaathiri  sana wasichana. Kwa kawaida kipindi cha balehe vijana wote wa kike na kiume vichocheo au homoni za kiume ‘Androgens’ huwa juu sana hivyo kusababisha tezi jasho, kutoa majimaji ya mafuta ‘Sebum’ kwa wingi.

Mabadiliko ya vichocheo katika utu uzima hutokea hasa kipindi cha hedhi siku chache kabla ya kuanza damu ndipo mwanamke hutokwa na chunusi nyingi ambazo hutoweka kabisa anapomaliza hedhi ingawa ni kwa muda mfupi, lakini hali ya chunusi usoni na sehemu nyingine huwa mbaya sana. Vichocheo vya mwili hubadilika pia mwanamke anapotumia dawa za uzazi wa mpango endapo anatumia vidonge, chunusi hutokea kwa wingi sehemu ya paji la uso na mashavuni na huisha akiacha kutumia dawa hizo.

Chanzo kingine cha chunusi ni kwa wale wanaotumia dawa za matatizo ya akili kama ugonjwa wa kifafa na sonona. Dawa hizi huchangia kuamsha chunusi. Matumizi ya vipodozi, mfano make-up huchangia kukuletea chunusi. Chunusi pia hufuata familia kama kwenu kuna watu wanasumbuliwa sana na chunusi.

USHAURI

Ili kuweza kukinga au kutibu chunusi, ni vizuri uzingatie usafi wa uso kwa kusafisha angalau mara mbili kwa siku bila kusugua sana ‘scrubbing’ muone daktari wako akuchunguze aina ya chunusi ulizonazo na akupatie dawa. Siyo kila dawa inatibu chunusi, zingine zinaharibu ngozi, pata ushauri wa kitaalam juu ya matumizi ya vipodozi hasa ’make-up’  ili usiharibu ngozi yako.

Tumia mafuta ya asili ili kujikinga na kutibu uso, mfano mafuta ya mwarobaini au aloevera au mchanganyiko wake kutegemea na ngozi yako. Wahi hospitalini kwa uchunguzi na tiba. Kwa kuangalia maelezo haya, hakuna uhusiano wa kutoshiriki ngono na chunusi. Ni imani potofu kuamini hivyo kwamba ngono ni suluhisho la chunusi.


Loading...

Toa comment