The House of Favourite Newspapers

Chuo Kikuu cha Tumaini Dar Chaanzisha Masomo ya Masters

0
Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (TUDARCo), Prof. Andrew Mollel (katikati) akizungumza na wanahabari wakati wa kutangaza kuanza kwa udahili wa wanafunzi wa masomo shahada ya uzamili chuoni hapo.

 CHUO Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (TUDARCo) kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani kimeanzisha rasmi udahili wa wanafunzi wa masomo ya Shahada ya Uzamili (Masters) ya Uongozi wa Biashara (Masters in Business Administration) na Shahada ya Uzamili ya Taaluma ya Habari (Master of Arts in Information) ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Global Group ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (TUDARCo), Eric Shigongo, akizungumza na wanahabari wakati wa kutangazwa kuanza kwa udahili wa wanafunzi wa masomo shahada ya uzamili chuoni hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Januari 22, 2020,  katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Makampuni ya Global Group, Sinza-Mori jijini Dar es Salaam, wakati wa kutangaza udahili huo, Naibu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Andrew Mollel, amesema kuwa wameanzisha programu hiyo kwa ajili ya kuwasaidia walioajiriwa, waliojiajiri na wote ambao hawana muda wa kutosha kuanzia asubuhi mpaka mchana, hivyo wataweza kusoma masomo hayo jioni.

“Tumepewa hadhi ya kutoa shahada ya uzamili  ya Taaluma ya Habari na shahada ya uzamili na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ambapo kutokana na masomo hayo tunakusudia kuwajengea umahiri wahitimu  katika uendeshaji wa habari za kidijitali, uendeshaji wa miradi ya habari, uendeshaji na utunzaji wa habari, pamoja na utengenezaji wa mifumo ya huduma za habari.

Dkt. Mollel akiendelea kufafanua masuala mbalimbali.

“Pia, uandaaji wa mifumo ya habari na uendeshaji wake, uchambuzi wa habari na mitandao ya kijamii, na kwa upande wa shahada ya uzamili ya Uongozi wa Biashara kozi itakuwa na michepuo ya Ujasiriamali na Masoko, Usimamizi wa Raslimali Watu, Fedha na Shughuli za kibenki.

Wanahabari wakifuatilia mkutano huo kwa makini kwani masomo hayo yanawahusu moja kwa moja.

“Pia, mwombaji awe na sifa zifuatazo katika kozi zote mbili, awe na Shahada ya Awali (Bachelor Degree) yenye ufaulu wa wastani wa GPA ya 2.7 kutoka chuo chochote kinachotambulika na serikali, awe na Stashahada ya Uzamili (Postgraduate Diploma) yenye ufaulu wa wastani wa GPA ya 4.0.

 

“Mwombaji mwenye shahada isiyo bainifu (unclassified degree) kama vile Shahada ya Sayansi ya Tiba (MD) anapaswa awe na angalau ufaulu wa daraja B katika somo alilomakinikia (Subject of Specialization).

 

“Aidha, mwombaji mwenye shahada ambayo ubainifu wake hautambuliki kwa urahisi na chuo itapaswa kupeleka vyeti au sifa zake  TCU, ili kupata utambuzi kabla hajafikiriwa kutahiniwa. Tunawakaribisha wote kutuma maombi ambapo mwisho wa kupokea ni Februari 28, 2020,  na masomo yataanza  Machi 16, 2020,” alisema Prof. Mollel.

Mkurugenzi wa Masomo ya Juu wa TUDARCo, Dkt. Peter Mtesigwa,  akizungumza na wanahabari.

Naye Mkurugenzi wa Masomo ya Juu katika chuo hicho, Dkt. Peter Mtesigwa alisema; “Watu wanaofanya kazi maofisini na wangependa kupata elimu ya jioni, tunafundisha kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 3:00. Kutakuwa na mihula mitatu, mihula miwili itakuwa ni ya darasani na muhula mmoja utakuwa ni kwa ajili ya utafiti, hivyo tunawakaribisha watu wote ili waweze kujipatia elimu iliyo bora.”

Mkuu wa Idara ya Habari na Ukutubi wa TUDARCo, Dkt. Getrude Ntulo, akifafanua jambo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Ukutubi wa chuo hicho, Dkt. Getrude Ntulo,  alisema anawakaribisha watu wote wenye vigezo husika ili kujipatia taaluma itakayowasaidia katika shughuli za kihabari.

 

“Mwandishi anaweza kuwa na habari lakini akashindwa kuifikisha kwa jamii kwa kufuata kanuni na maadili ya taaluma. Hivyo,  tutawafundisha vizuri namna ambavyo habari zinatakiwa kufikishwa kwa jamii. Chuo kipo Mwenge Barabara ya Coca Cola,” alibainisha Dkt. Ntulo

Stori: Neema Adrian na Richard Bukos | GPL

 

Leave A Reply