The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-25

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:

Baba Shua alimkuta mama Shua sebuleni akiwa katika hali ya kutojua nini kinaendelea. Aliingia chumbani bila kusalimia, akapanda kitandani kulala maana alishaoga nyumbani kwa Maua na kupakwa mafuta ya losheni na pafyumu juu.

TAMBAA NAYO…

Kitendo cha baba Shua kumpita kama hamuoni kilimuumiza akili mama Shua, akahisi kama kuna la ziada ya pale…

“Afadhali hata angenisalimia lakini kunipita kasi bila salamu maana yake nini sasa?” alijiuliza mama Shua.
Alijishauri kuhusu kumfuata au kutomfuata mumewe, chumbani lakini mwisho wa yote aliona itakuwa ujinga kumfuata…

“Yaani kumtenda kote kule halafu nimfuate? Je, akinipiga nitasema amenionea? Pengine karudi bado na hasira, kaepusha mabaya kwa kwenda chumbani halafu eti nimfuate, si itakuwa naendekeza ushetani!”
***
Kule chumbani akiwa tayari kitandani, baba Shua naye aliwaza yake kwamba, endapo mama Shua atamuibukia chumbani salama yake afikie kulala. Lakini akisema amuulize kwa nini hajamsalimia, atavaa na kuondoka zake kurudi kwa Maua…

“Tena kwanza ngoja nimpigie simu Maua, aliniambia nikifika nimjulishe,” alisema moyoni baba Shua, akashika simu yake na kumwendea hewani Maua lakini wakati huohuo, mama Shua naye akaingia kwa lengo la kupanda kitandani kulala…

“Ee mambo vipi? Umelala nini..? Bado..? Oke…mimi ndiyo nipo kitandani muda huu…nilisema nitakupigia nikiwa nimejilegeza kitandani…usijali…aaa! Wewee…wewee! Mmmh! Acha bwana…teh…the! Haya poa…na wewe pia…aaaa bwana acha mambo yako wewe…oke oke.”
Mama Shua alifuatilia sana mazungumzo hayo ili kujua mumewe anaongea na nani kwenye simu. Kwa mbali alihisi anaongea na mwanamke, lakini pia akahisi ni mwanaume, hasa kwenye vile vipengele vya ‘acha bwana…oke oke poa.’

Baba Shua naye akawa anamuwaza Maua na maneno yake ya kwenye simu…
“Mh! Maua bwana…ei nibusu…hivi anavyoamini ningembusu kweli? Ingewezekana wapi kwanza? Ye anajua mke wangu atakuwepo sasa ningembusu vipi? hata kama kweli tumerudisha majeshi nyuma lakini si kwa kiasi cha kuleta ubaya. Mbaya aachwe na ubaya wake.”

Usiku wa siku hiyo ulikuwa mrefu kwa wote wawili lakini kila mmoja alikuwa akiwaza yake.
Mama Shua yeye aliwaza maisha yatakavyokuwa baada ya kutoka kwa baba Shua kutokana na hali ilivyokuwa wakati baba Shua yeye alikuwa akiwaza maisha yake na Maua…
“Siamini kama atanitenda kama mama Shua…kwanza Maua hata tulipokuwa klozdi enzi zile sikuwahi kumuwazia kwamba ananisaliti. Naamini si msaliti,” aliwaza baba Shua.
***
Kwake Maua mambo yalikuwa vilevile kama baba Shua. Muda mwingi alimuwaza mama Shua na uovu wake kwa mumewe hasa akizingatia kwamba, ndiye aliyevunja uhusiano wake na baba Shua…
“Mshenzi sana yule mwanamke. Yaani aliingilia penzi langu kumbe hawezi chochote. Haya sasa…ndoa imemshinda sijui atasemaje!”
***
Baba Shua alilala usingizi mzito siku hiyo, tena akikoroma jambo lililomshangaza sana mkewe mama Shua kwani alitarajia kuwa, kutokana na mambo yaliyotokea, angelala kimang’amumang’amu.
“Mh! Yaani baba Shua pamoja na mambo yote yaliyotokea, bado analala usingizi kweli? Ina maana kitendo changu hakijamkera? Mbona mi mwenyewe nimekereka?” alijiuliza mama Shua bila kupata majibu. Mpaka kunakucha, mama Shua hakuwa amelala usingizi unaoeleweka.
***
Kulikucha, mama Shua alitoka kitandani, akaenda uani kufanya kazi za usafi huku akiwa ametenga maji ya kuoga kwa ajili ya mumewe baba Shua.

Lakini baba Shua akiwa kitandani hajatoka bado lakini alishaamka, akaanza kuchati na Maua…
“Mambo baby, ndiyo naamka mimi,” alituma ujumbe huo baba Shua…
“Ooh! Thanx God kwa ajili ya wewe! Mimi nimeshaamka. Ila natamani sana kama ungekuja kuoga kwangu kabla ya kwenda kazini…”

“Da! Nguo sasa ndiyo tatizo mama…”
“Nguo! Si utabeba za kuvaa baada ya kuoga.”
Baba Shua aliamini ni ushauri mzuri hasa akizingatia kwamba, hana mawasiliano pale kwake zaidi ya msichana wa kazi na binti yake Shua.

Alitoka kitandani, akachukua begi dogo la mgongoni, akaingiza suruali moja, singilendi moja na shati moja, viatu na soksi alivaa kabisa, akaondoka zake bila kuaga mtu.
Wakati anaondoka, mama Shua alikuwa uani. Alijua mumewe angeenda kuoga lakini alipoona kimya, akaingiwa na wasiwasi, akaenda chumbani na kukuta kiasi cha pesa juu ya meza, lakini baba Shua hakuwepo…
“Khaa! Huyu kaenda wapi tena?” alijiuliza. Alimwamsha Shua na kumuuliza lakini alionekana hajui lolote maana alikuwa usingizini.

Aliingiwa na wasiwasi kwamba, huenda ameamua yeye ndiyo ahame kwenye nyumba hiyo na kumwacha yeye na Musa wake, lakini alipofungua kabati la nguo hakuona mabadiliko. Wingi wa nguo ulikuwa uleule na haikuwa rahisi kubaini kwamba, mumewe ametoka na begi lenye nguo chache.
Hata alipokwenda kwenye sehemu ya viatu alibaini kuwa, ni pea moja tu haipo kwa tafsiri rahisi ni kwamba ndivyo alivyovaa…

“Mh! Mimi sijui sasa,” alijisemea moyoni kama vile aliisikia sauti kichwani ikimuuliza.
Alitoka nje na kukuta na Musa naye akiwa ametoka ili akaoge…
“Mambo?” Musa alisalimia.
“Poa tu,” mama Shua alijibu kwa mkato sana huku akichukua tahadhari kwa lolote endapo mumewe angetokea na kuhisi vibaya.

Akili haikumpa mama Shua, akaamua kumpigia simu baba Shua lengo ni kutaka kujua aliko lakini simu yake iliita kwa muda mrefu sana bila kupokelewa.
Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.

Baba Shua aliiona simu hiyo ya mkewe lakini hakuona sababu ya kuipokea…
“Kwanza niipokee ili iweje? Najua anataka kujua kuhusu nilipo, halafu akishajua ili iwe nini? Mbona mimi sitaki kujua mambo yake?” alisema moyoni baba Shua na ili kupangua simu ya mkewe, alimpiga mabusu Maua mpaka wakajikuta wakiangukia kwenye kochi kubwa…

Leave A Reply