The House of Favourite Newspapers

Corona Inatisha! Kufungwa Makanisa Msikitiki Itakuwaje?

0

WAKATI tishio la virusi vya mafua ya Corona likizidi kushika kasi nchini na mataifa mengine kibao, suala la makanisa na misikiti kufungwa nalo limetikisa, Amani linakupa habari kamili.

 

Baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufunga kwa siku 30 shule kuanzia zile za awali mpaka vyuo vikuu kutokana na tishio hilo la Corona mjadala mzito uliibuka kwenye mitandao ya kijamii na mitaani kwamba kinachofuata ni kufungwa kwa nyumba za ibada.

 

Mjadala huo ulieleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa nyumba za ibada kufungwa kama walivyofanya nchi za nje kama Saud Arabia na Vatican kwa sababu mikusanyiko hairuhusiwi kwa sasa.

 

Watu hao walienda mbali zaidi na kujiuliza kuwa endapo makanisa na misikiti itafungwa watu watamuomba Mungu wakiwa wapi? Hali itakuwaje?

 

Kutokana na mjadala kuwa mkubwa, Amani liliwatafuta baadhi ya viongozi wa dini ambao kila mmoja alizungumza lake huku wakiwataka Watanzania kuzidi kumuomba Mungu ili auondoe kabisa ugonjwa huu wa Corona.

 

SHEHE ALHAD MUSSA SALUM

“Sisi kama viongozi wa dini tumepokea maelekezo ya Waziri Mkuu, maelekezo ya Wizara ya Afya na maelekezo ambayo yanaendana na mafundisho ya dini zetu.

 

Tumetoa tamko kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima kama shughuli za Maulid mtaani, harusi pia tumefunga madrasa zote, tumetoa maelekezo misikitini kwamba watu wakifika wanawe vizuri kwa sabuni.

 

“Na tumeshauri watu watie udhu majumbani mwao kabla ya kwenda msikitini ili kuepusha ule msongamano hivyo misikiti haiwezi kwa sababu watu wanafuata utaratibu.

 

“Maagizo yametolewa kupitia kwa Mufti wa Tanzania, Issa Shaaban Simba kwamba misikiti yote iendelee kutoa dua ambapo kila baada ya sala inafanyika,” alisema Shehe Mkuu wa mkoa wa Dar.

 

ASKOFU RUWAI’CHI

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki, Dar Es Salaam, Yuda Thadeus Ruwai’chi alisema huu ugonjwa ni hatari hivyo wao kama viongozi wanajitahidi kuwahimiza na kuwasihi waumini wao kuzingatia na kufuata sheria ambazo zinatolewa na wataalamu pamoja na viongozi ili wasikumbwe na ugonjwa huo.

 

“Kuhusu makanisa kufungwa hiyo haiwezekani bali kikubwa tunazidi kufuata taratibu zinazotolewa na wataalamu wa afya naamini Mungu atatuvusha tu kwenye hili.

 

“Tunajitahidi sana katika kuwahimiza waumini wetu kuzingatia taratibu ambazo zinatolewa na vyombo husika vya afya, wakizingatia hivyo tunaamini kwamba mambo yataenda sawa na hakuna kanisa litakalofungwa.”

 

ASKOFU MWAMALANGA

Kwa upande wa Askofu William Mwamalanga ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maadili ya amani na haki za binaadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini hapa nchini alisema anasikitishwa sana na Corona kwa sababu ni hatari hivyo kuiomba Serikali kuwashughulikia wale wote ambao wanajiita manabii wa Corona kwa sababu siyo kweli bali wanadanganya wananchi.

 

“Huwezi kufunga nyumba za ibada maana ni kama vile sasa unaruhusu kirusi hicho kiingie ila ukifunga shule na vitu vingine ni sawa, hivyo ibada zitaendelea kama kawaida lakini tutazingatia sheria zinavyosema, mfano sasa hivi kuna utaratibu tunasambaziana kwamba watu wanapoingia kanisani kila mtu akae kwenye eneo la wazi (waachiane nafasi vizuri) .

 

“Na wanapoingia wagonjwa kwa ajili ya kuombewa, watengewe eneo lao ili baada ya maombi kanisa liwapeleke hospitali yeyote iliyopo karibu, pia lazima uwepo kuweka maji yenye dawa za kuua hivyo virusi,” alisema Mwamalanga.

 

NABII BUKUKU

Nabii Esther Bukuku wa Kanisa la Prophetic Ministry International (PMIC) alisema suala la makanisa kufungwa si hoja sana kwa sababu hata makanisa yakifungwa pointi itabaki Mungu anatutaka sasa tumrudie yeye na kila mmoja aombe kwa imani naye siyo kupigana vijembe na kugombea dini au vyeo vya dini.

 

“Tuwe tayari kusikiliza nabii wa Mungu kwa sababu hakuna njia nyingine tunaweza kusikia Mungu anasema nini bila kusikia sauti ya nabii wake na tukifanya hivi dunia na Tanzania yetu kwa jumla itakuwa salama na haya tuyaonayo yatapita.”

 

NABII NYAKIA

Nabii Nyakia wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda, Dar alisema ndani ya kanisa lake wana maombi maalumu ya wiki nzima ya kuomba Mungu aliondoe janga hili.

 

“Nyumba za ibada kufungwa itakuwa ni vigumu maana kuna madhara makubwa yatatokea kwani linapotokea tatizo ndiyo wakati hasa wa watu kumuomba Mungu, sasa zikifungwa si itakuwa harari zaidi, ndiyo maana tuna maombi maalumu ya kutokomeza kabisa ugonjwa huu.”

Stori: Memorise Richard, Amani

Leave A Reply