Rosa Ree: Sina Mpango Na Kiki

MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Rosery Robert ‘Rosa Ree’ ambaye anatamba na Ngoma ya Nazichanga ameeleza kuwa katika kazi yake hiyo hana mpango wa kufanya kiki kama wafanyavyo wasanii wenzake.

 

Mwanadada huyu alijipatia umaarufu kwa staili yake ya kuchana kama alivyofanya kwenye ngoma zake za Dip N Whine, Banjuka, Acha Ungese, Asante Baba, Up In The Air pamoja Nguvu za Kiume.

 

Akipiga stori na Showbiz , Rosa Ree alisema kufanya kiki kwake anaona ni kujishushia ufanisi na kipaji alichonacho kwani kinatosha kabisa kufanya kazi yake ibambe kila kona.

Rosa Ree amezungumza mengi, ungana naye hapa chini;

 

Showbiz: Muziki wa sasa umetawaliwa na kiki, kwako hili likoje?

Rosa Ree: Siamini katika kiki na sina mpango wa kufanya kiki, ingekuwa kama nataka ningefanya sana ila sipendi kwa sababu kila kitu namtegemea Mungu tu yeye ndiye anainua muziki wangu.

Showbiz: Mipango yako kwa mwaka huu ikoje?

 

Rosa Ree: Nimejipanga kuachia albamu yangu pamoja na timu yangu na kuna nyimbo ambazo zipo tayari.

Showbiz: Kwa nini umeamua kutoa albamu?

Rosa Ree: Ni miaka mingi sana watu wananiuliza lakini nilikuwa nashindwa kwa sababu sipendi kufanya kazi kwa kukurupuka yaani unakuwa kama bendera fuata upepo, hivyo mwaka huu niko tayari kuwapa mashabiki wangu walichokitaka kwa muda mrefu.

 

Showbiz: Albamu yako ina nyimbo ngapi?

Rosa Ree: Ina nyimbo 10 ila kama zikiongezeka mtanisamehe kwa sababu siwezi kujua hapo mbele itakuwaje kwa sababu sisi wasanii hatutabiriki, ukijisikia kuongeza unaongeza.

Showbiz: Kwenye hiyo albamu yako kuna wasanii umeshirikiana nao?

 

Rosa Ree: Ndiyo, kuna wasanii wa nje na ndani, siwezi kuwataja mpaka pale tukiwa tayari tutatoa listi ya ngoma na majina yake.

Showbiz: Je, una mpango wa kubadili mtindo wako wa kuimba?

 

Rosa Ree: Ndiyo na kuna ngoma ambayo nilishawahi kuimba hapo kabla naweza kuchana na kuimba maana napenda kujichanganya kwenye aina tofautitofauti.

Showbiz: Wasanii wengi kwa sasa wameamua kugeukia Singeli wakiwemo wa Hip Hop mfano Chemical, je kwako imekaaje hii?

 

Rosa Ree: Sijawahi kuwaza kuimba Singeli, sisemi kwamba eti siwezi bali ni kwamba; sifanyi mambo kwa kuiga na kufuata mkumbo maana ni kitu ambacho siyo kizuri, siku mkumbo ukizima na wewe unazima, hivyo napenda kufanya vitu venye ubora tu na si vinginevyo mfano mzuri muziki wa Jay Z unasambaa ulimwenguni kote kwa sababu anafanya vitu venye ubora wa kutosha.

 

Showbiz: Kuhusiana na kazi za kimataifa, ulishawahi kutamani kufanya kazi na Jay Z maana anafanya muziki unaokubalika ulimwenguni?

Rosa Ree: Ndiyo tena sana kwa nini nisiwaze kufanya naye kazi? Kwa sababu Jay Z ni role model wa wasanii wengi duniani kutokana na kazi zake kukubalika kila sehemu.

 

Showbiz: Inasemekana wewe ni mwanamke ambaye hutaki mchezomchezo, mtu akikuchokoza wewe ni ngumi mkononi, unazungumziaje?

 

Rosa Ree: Lazima watu wawe na taswira fulani kwenye akili zao kuhusiana na mimi ila sipo kwa ajili ya kubadilisha taswira zao nipo kwa ajili ya kufanya kazi, wenyewe wakisema hivyo ni sawa tu kusemwa ni kawaida kwa mwanadamu, kingine mimi ni mdada wa Arusha hatuna mchezo nadhani watu wanafahamu hilo.

 

Showbiz: Mbali na muziki unajishughulisha na nini?

Rosa Ree: Nafanya biashara, nina supermarket yangu mwenyewe.

Showbiz: Kwa upande wako ulishawahi kuwaza au kuwa na mpango wa kuingia kwenye filamu?

 

Rosa Ree: Nikipata dili nono nitaigiza tena haraka sana kwa sababu naamini watu watafurahi.

Showbiz: Umewahi kuwa chini ya menejimenti tofautitofauti ikiwemo The Industry ya Navykenzo, vipi kwa sasa uko chini ya menejimenti ipi?

 

Rosa Ree: Ndiyo nimewahi kuwa kwenye lebo tatu tofauti lakini kwa sasa hivi nipo kwenye lebo ambayo ni watu wangu wa karibu sana namaanisha familia yangu ndiyo ambao wananisimamia pia nashukuru sana Mungu kwa kunipa familia kama hii.

 

Showbiz: Akitokea mtu tofauti akataka kukumeneji utakubali?

Rosa Ree: Hapana yaani labda aje na mabilioni ya fedha ila kumkubalia haitakuwa rahisi.

Showbiz: Neno la mwisho kwa mashabiki wako ni lipi?

Rosa Ree: Nawapenda sana, kikubwa wazidi kunisapoti.

Toa comment