The House of Favourite Newspapers

Corona: Mwanri Asimamisha Likizo za Waganga, Wauuguzi

0

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, amesimamisha kwa muda likizo za watumishi wakiwemo wa idara za afya ili waendelee kuunganisha nguvu katika kusaidia jamii kwenye kampeni za mapambano ya ugonjwa wa Covid -19.

 

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kunakuwepo wataalamu wa kutosha katika maeneo yote ambao wataendelea kutoa elimu ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi aina ya Corona usiingie mkoani Tabora.

 

Mwanri alitoa kauli hiyo wilayani Uyui na Nzega wakati ziara yake ya kukagua vituo na zahanati zilizoandaliwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa huo kama itatokea wakaonekana Mkoani humo.

 

Alisema kipaumbele hivi sasa ni kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa ili wakazi wa Mkoa wa Tabora waendelee kuwa salama kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na viongozi wa kitaifa.

 

Aidha, Mwanri alizitaka Halmashauri zote  kutumia redio zilizopo na magari ya matangazo kupeleka elimu katika maeneo mbalimbali ya wananchi juu ya kujikinga na kujilinda dhidi ya Covid -19.

 

“Tumieni magari yenye vipaza sauti kupita katika mitaa mbalimbali kutoa elimu ya kujikinga wakati wote…na pia wataalamu nendeni katika redio zote zilizopo mkoani Tabora kupeleka ujumbe ambao utawasaidia wananchi kuepuka kupata maambukizi ya Corona,” alisema.

 

Katika hatua nyingine Mwanri ameziagiza halmashauri zote kuhakikisha magari yote ya abiria yanayosafirisha abiria ndani na nje ya  Tabora yanapuliziwa dawa kabla ya safari ili kuwakinga abiria dhidi ya uwezekano wa kupata corona.

 

Alisema ni lazima gari linapofika stendi lipuliziwe dawa na taarifa zake zijazwe kwenye fomu ili kuonyesha kuwa limetekeleza agizo hilo ndipo liruhusiwe kupakia abiria na kuendelea na safari zake.

Leave A Reply