The House of Favourite Newspapers

Rais Putin ‘Ajificha’ Kupambana na Corona

0

RAIS  wa Urusi, Vladimir Putin,  kuanzia sasa atakuwa akifanya kazi akiwa nyumbani kwake huko Novo-Ogarevo, karibu na jiji la Moscow, msemaji wa Kremlin amesema siku moja baada ya daktari aliyekutana na rais huyo  wiki iliyopita kupatikana na virusi vya Corona.

 

Kiongozi huyo wa Urusi anatarajiwa leo mchana kuongoza mkutano wa wajumbe wa serikali yake kwa njia ya video, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari, akibainisha  kwamba  Putin, ambaye kwa mujibu wa Kremlin yuko katika afya njema, sasa ameamua kufanya kazi akiwa nyumbani kwake.

 

“Kila mtu sasa anajitenga na wengine kutokana na hali inayojiri kwa sasa,”  Peskov ameongeza.

Visa 2,777 vya maambukizi ya virusi vya Corona vimethibitishwa nchini Urusi ambapo watu 24 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo ambao ulianzia nchini China mwezi Desemba mwaka 2019, kabla ya kusambaa katika zaidi ya nchi 200 kote ulimwenguni.

 

Katika kujaribu kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo,  hasa katika mji mkuu, ambao umekuwa kitovu cha janga hilo nchini humo, siku ya Jumapili Manispaa ya Jiji la Moscow ilitangaza marufuku kwa watu kutoka nje ya makazi yao.

Leave A Reply