The House of Favourite Newspapers

Corona Yaleta Mtikisiko Wa Uchumi Dunia Nzima

0

DAR: Ni vilio kila kona, ndivyo unavyoweza kutafsiri janga la maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo sasa vimeathiri sekta zote duniani huku sekta ya uchumi ikitajwa kuporomoka zaidi kwa kasi katika kipindi cha mwaka huu.

 

Kusambaa kwa Virusi vya Corona katika nchi 194 duniani kumeendelea kuleta mtikisiko wa kipekee katika nyanja ya uchumi hasa ikizingatiwa nchi zilizoathiriwa pakubwa na ugonjwa huo wa COVID -19 zimefunga shughuli zote na kuagiza wananchi wake kusalia ndani kwa muda wa siku kadhaa.

Hali hiyo imetajwa kuathiri sekta ya uzalishaji ambayo sasa Shirika la Kazi Duniani (ILO) limesema watu milioni 25 watapoteza nafasi zao za kazi au ajira.

 

Ripoti hiyo iliyotolewa Machi 23, mwaka huu, imesema mlipuko wa Covid-19 umepunguza kwa kiasi kikubwa nafasi za ajira duniani, sambamba na kupunguza mishahara na marupurupu kwa wafanyakazi.

Mkurugenzi wa ILO, Guy Rider alisema janga hilo siyo tu limeleta mgogoro wa kiafya duniani, lakini pia ni janga kubwa katika soko la ajira na mgogoro wa kiuchumi ambao umekuwa na athari kubwa kwa watu wa kada zote.

 

“Kuna uwezekano wa kutokea mtikisiko mkubwa zaidi wa kiuchumi kama ilivyo katika sekta ya afya kama tusipochukulia suala hili kama letu sote, bila shaka haya yatatokea kama ilivyokuwa kwenye hali mbaya ya uchumi duniani kote mwaka 2008/2009, lakini kama hatua hizi zisipochukuliwa kuna uwezekano wa watu wengi kupoteza ajira,” ilisema.

 

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara (UNCTAD), Richard Kozul ambapo alisema uchumi utashuka kwa asilimia mbili na kugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani trilioni moja kuziwezesha nchi zilizoathiriwa kusimama tena kiuchumi.

Akizindua ripoti ya shirika hilo mapema wiki hii sekta kubwa kama vile za uzalishaji wa mafuta, usafiri na huduma nyingine muhimu zimeathiriwa na kusambaa kwa virusi hivyo.

 

TANZANIA ITAATHIRIWA HIVI

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Romanus Dimosso alisema virusi hivyo vitaathiri uzalishaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwamo kilimo, viwanda na huduma.

“Sekta zote hizi zitaathirika kwa mfano uchukuzi, shirika la ndege Tanzania limenunua ndege juzi tu, lakini sasa hakuna abiria, kwa sababu nchi nyingi zimefunga huduma hizo, hawataki abiria waingie kwenye nchi zao.

 

“Kwa mfano safari za Mumbai, China na Afrika Kusini, kote tumezipaki. Pia usafiri wa ndani abiria wamepungua sana. Nilikuwa Mwanza nimerudi hapa Mzumbe, ndege ilikuwa na abiria nusu,” alisema.

“Hiki ni kitu ambacho kimetokea kwa dharura, athari zake tusipojipanga mapema zitaleta athari kwenye afya za watu,

“Kwanza serikali iendelee na mikakati kuhakikisha raia wanakuwa na afya nje kuepuka vifo na magonjwa.

 

“Pili, raia tusichukulie kama tumepata likizo, popote linapowezekana kufanyika lifanyike, katika sekta ya huduma kama elimu, mashule yamefungwa, walimu wanaweza kufanya kazi kwa kutumia Tehama.

“Kuna miundombinu ya kujifunza kwa masafa ya matandao, badala ya kukaa wamejifungia ndani na kucheza,” alisema.

 

PROF LIPUMBA

Aidha, mtaalam wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Ibrahim Lipumba naye aliunga mkono hoja hiyo na kubainisha kuwa uzalishaji utapungua kadiri watu watakapoacha kufanya kazi.

Alitolea mfano kuwa shule zimefungwa, lakini walimu wanaendelea kulipwa mishahara.

“Shule binafsi zikifungwa watoto hawaendi shule, wazazi wakishindwa kulipa ada na mishahara itakuwa shida. Mahitaji yatapungua kwa sababu watu wakiwa hawana pesa hawatanunua kitu.

 

“Pia bei za bidhaa tunazouza nje, kwa mfano pamba, korosho, kahawa na karafuu bei yake itaporomoka, fedha za kigeni tunazopata zitapungua, kwa hiyo inategemea namna ugonjwa ulivyoathiri,” alisema.

Alisema tatizo ni kwamba chanzo cha mapato ya Watanzania wengi siyo rasmi.

 

“Watu wanategemea kipato cha kila siku, usipotoka au ukiugua hata hela ya chakula huwezi kuwanayo, athari zake huwa ni kubwa mno kukiwa na hali kama hiyo.

“Hosptali za kukidhi mahitaji kwa mfano Kenya taarifa zinaonesha wana vitanda vya ICU 500 nchi nzima, kwa hiyo na sisi hatutakuwa mbali na takwimu hizo, sasa watu wakiugua kwa wingi itakuwaje?” Alihoji.

 

WAFANYABIASHARA

Aidha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabishara Kariakoo, Abdallah Mwinyi, alisema kiujumla kwa sasa hali ya biashara ni mbaya kwa sababu mzunguko wa fedha na bidhaa umesimama.

“Watu wana marejesho benki na kwa sasa watu wanauza bidhaa zilezile za nyuma huku wanalipa kodi, umeme, marejesho ya benki na mengineyo.

 

”Wakati ugonjwa huu unatokea ni kipindi ambacho kilikuwa ni Sikukuu ya Wachina ambapo huwa viwanda vyote vinafungwa na wanapokua wanafunga hakuna mzigo wowote unaozalishwa kwa hiyo hali ni mbaya sana maana kwenda nchini nyingine kama Uturuki bei ni ghali,” alisema.

 

NINI KIFANYIKE?

Kutokana na hali hiyo, Shirika la Kazi Duniani la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za dharura katika ngazi za kitaifa na kimataifa ili kupunguza athari hasi za mlipuko wa Corona kwa sekta ya ajira.

Dk Romanus alisema kwa kuwa Ugonjwa wa COVID-19 umetokea kwa dharura, athari zake Serikali inatakiwa kuendeleza mikakati ya kuudhibiti ili usilete athari kubwa kwa Watanzania.

 

“Kwanza Serikali iendelee na mikakati kuhakikisha raia wanakuwa na afya nje kuepuka vifo na magonjwa. Pili raia tusichukulie kama tumepata likizo, popote linapowezekana kufanyika lifanyike, katika sekta ya huduma kama elimu, shule zimefungwa, walimu wanaweza kufanya kazi kwa kutumia Tehama,” alisema.

 

Alisema kuna miundombinu ya kujifunza kwa masafa ya matandao, badala ya walimu kujifungia ndani na kucheza bao, watumie Tehama kutekeleza majukumu yao.

Kutokana na hilo, alisema Serikali inapaswa kutoa kauli kwa taasisi za fedha, hasa benki ili wafanyabiashara wapewe kipindi cha mpito kulipa marejesho.

 

Naye Mwinyi Ali alisema Serikali inatakiwa kutoa uamuzi kwenye taasisi za fedha, yaani benki ili wafanyabiashara wapewe kipindi cha mpito kuhusu muda wa marejesho.

“Tunaiomba Serikali ifanye jambo kwa taasisi hizi za fedha,” alisema Mwinyi.

Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa

Leave A Reply