The House of Favourite Newspapers

Corona Yatibua Fumanizi la Mwaka!

0

MOROGORO: UKISIKIA Corona imetibua fumanizi, ndio hili lililotokea mkoani Morogoro na kuwanyima wakazi wa mji huo kushuhudia uhondo wa mshikemshike wa fumanizi baada ya Serikali kuzuia mikusanyiko ili kupunguza maambukizi ya Virusi hatari vya Corona.

Fumanizi hilo ambalo limetokea Aprili 22 mwaka huu, muda wa saa 8 mchana kweupe katika Mtaa wa Polisi Kota Mkoani Morogoro.

 

TUKIO LILIVYOKUWA

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, wambea walimtonya Paparazi wetu na kutinga eneo hilo la tukio ambalo lipo katikati ya mji jirani na ofisi za kikosi cha Jeshi la Zima Moto na Uokoaji.

Alipotua alishuhudia mume aliyemfumania mkewe akimlazimisha mkewe kupanda bodaboda wakayamalize nyumbani akiogopa kujaza mkusanyiko, akidaiwa kuhofia Corona.

 

Kwa hofu ya dhambi aliyotenda mwanamke huyo, aligoma kupanda bodaboda hiyo kama alivyoamuliwa na mumewe. Kitendo hicho kilimkera mwanaume huyo na kuamua kumpakia ‘mshikaki’ kinguvu na kuondoka naye.

 

MASHUHUDA WATEMA UBUYU

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walilieleza RISASI kuwa, hilo ni fumanizi la aina yake kutokana na mazingira pamoja na uamuzi ambao mume ameamua kuuchukua.

 

“Jamaa kamfumania mshikaji akiwa geto na mkewe, cha ajabu hakufanya vurugu yoyote. Aliamua kumchukua mkewe na kumpakia kwenye bodaboda na kuondoka zake huku akimuacha huru mgoni wake! Ni jambo la kushangaza sana maana tumezoea kuona mafumanizi kama haya lazima angetolewa ngeu huyo mgoni,” alisema Juma ldd ambaye ni Fundi wa masofa.

 

MWENYEKITI AFUNGUKA

Kaimu Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Polisi Kota, Amina Kimaro amethibitisha kutokea kwa fumanizi hilo kwenye mtaa wake.

 

“Ni kweli fumanizi hilo limetokea hapa mtaani kwangu, tena nyumba ya pili kutoka kwenye nyumba yangu na fumanizi hilo halikuchukua hata dakika 20, mume ambaye sio mkazi wa mtaa huu alimchukua mkewe wakapanda bodaboda wakaondoka huku watu wengi wakihofia kujazana eneo la tukio kutokana na tukio la maambukizi ya Corona,” alisema.

STORI:DUSTAN SHEKIDELE, RISASI

Leave A Reply