The House of Favourite Newspapers

Dakika 593 za Bocco Zampagawisha Kocha

0

NAHODHA wa Simba, John Bocco ‘Papaa’, amempagawisha kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, baada ya kukichafua katika Ligi Kuu Bara tangu amerejea kutoka kwenye majeruhi.

 

Bocco alikuwa nje ya uwanja tangu Agosti 18, mwaka jana baada ya kuumia kifundo cha mguu Agosti 17, 2019, kutokana na rafu mbaya aliyochezewa na kiungo mkabaji wa timu ya Azam FC, Frank Domayo kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambao Azam ilipoteza kwa mabao 4-2 dhidi ya Simba uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bocco alirejea uwanjani Januari 4, mwaka huu kwenye pambano la Simba na Yanga ambalo liliisha kwa sare ya mabao 2-2, ambapo katika mechi hiyo aliingia dakika ya 69 kuchukua nafasi ya Meddie Kagere ambaye aliifungia Simba bao la kwanza na katika dakika ya 89, Bocco aligongesha mwamba baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi safi iliyopigwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

 

Mpaka sasa Bocco amecheza michezo 10, ambazo ni sawa na dakika 593, ameanza kwenye kikosi cha kwanza katika mechi 6 ambazo ni dhidi ya Mbao FC, Coastal Union, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, Lipuli na Kagera Sugar huku akitokea benchi kwenye michezo minne dhidi ya Yanga, Alliance, Namungo na JKT Tanzania.

 

Tangu amerejea uwanjani, Simba imefunga mabao 18 huku akiwa amehusika katika mabao matano, amefunga mabao matatu dhidi ya Polisi Tanzania dk 57, Mtibwa Sugar dk 45, Lipuli dk 23 na ametoa asisti moja kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa bao ambalo lilifungwa na Hassan Dilunga dakika ya 58, amesababisha penalti moja dakika ya 59 ambayo alifunga Kagere dakika ya 61.

 

Hata hivyo Bocco ameweka rekodi ya kugongesha miamba mara nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote wa Simba kwenye mechi 10 alizocheza, Bocco amegongesha mwamba kwenye mechi ya Yanga dakika ya 89 na amegongesha mwamba dakika ya 74 kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar.

Abdulghafal Ally, Dar es Salaam

 

Leave A Reply