The House of Favourite Newspapers

Daktari Feki Anaswa Akitoa Huduma za Kibingwa

0

MKAZI wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Romu wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Othuman Kimaro, amekamatwa na vyombo vya dola akituhumiwa kujifanya daktari na kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa, zikiwamo zinazotakiwa kutolewa na madaktari bingwa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, aliagiza kukamatwa na kuhojiwa kwa Othuman baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kuzuru kwenye zahanati bubu inayodaiwa kutumiwa na mtuhumiwa huyo kutibu wagonjwa, huku akiwa hana leseni ya kufanya kazi hiyo.

 

“Sasa hivi kuna mtoto yuko Hospitali ya Rufani ya KCMC amelazwa kule akipatiwa matibabu kwa sababu ya mambo haya, OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya), TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) na Ofisa Mtendaji wa Kata hii. Huyu mtu ninawaachia hapa.

 

“Ahojiwe na aeleze kwa nini anahatarisha uhai wa watu? Anaweza kugharimu maisha ya watu hapa Mudio na kwingineko kwa kutoa huduma za tiba wakati hata serikali haimtambui.

 

“Anatoa dawa, anaandika rekodi za wagonjwa na anafanya kazi nyingine zinazostahili kufanywa katika ngazi ya vituo vya afya na hospitali za wilaya.

 

“Ana lundo la dawa hatari ambazo hazitakiwi kutolewa nje ya hospitali au vituo vya afya, ana vifaa na dawa za kuosha kizazi, maana yake anaweza kuwa ndiye kinara wa kufanya abortion (kutoa mimba),” Ole Sabaya aliongeza.

 

Alipoulizwa na kiongozi huyo kuhusu shughuli zinazoendelea kwenye nyumba aliyokutwa yenye dawa na duka la dawa, mtuhumiwa huyo alidai anatoa huduma za kifedha zinazotolewa kupitia miamala ya mitandao ya simu.

Leave A Reply