The House of Favourite Newspapers

Dalili na tiba ya ugonjwa wa presha ya macho!

MTU anaweza kujiuliza presha ya macho au kitaalamu Glaucoma ni nini? Hili ni ongezeko la presha ya macho, kimsingi macho huwa yana presha ya 10mmhg mpaka 21mmhg lakini inapozidi hapo mtu hutambuliwa kuwa ni mgonjwa wa presha ya macho.

Mara nyingi ugonjwa huu hurithiwa na hauonyeshi dalili zozote mpaka baadaye sana mtu anapokua mtu mzima.

Ugonjwa huu huathiri mishipa ya fahamu inayohusika na kuona kitaalamu huitwa optic nerve na mgonjwa asipokua makini na matibabu yake basi huweza kupata upofu wa moja kwa moja na asione tena maishani mwake.

 

CHANZO CHA UGONJWA

Kitaalamu upande wa mbele ya jicho kuna majimaji ambayo kitaalamu tunaita aquous homour ambayo kazi yake ni kuleta virutubisho kwenye sehemu za jicho iitwayo iris, lenzi na cornea.

Pia majimaji hayo huondoa mabaki ya matumizi ya virutubisho hivyo vilevile hutunza shepu ya jicho. Sasa majimaji haya yanapozidi ndio presha ya macho inapanda.

Kwa kawaida hali hii hurithiwa kutoka kwenye kizazi kimoja mpaka kingine na sababu zingine zinazoweza kuongeza presha hii ni magonjwa ya macho.

Kuumia jicho kwa kupigwa na kitu au kumwagikiwa kemikali au baada ya upasuaji wa macho wa kutibu tatizo lingine la macho ni moja ya chanzo kingine cha tatizo la jicho.

 

WENYE HATARI YA KUUGUA PRESHA YA MACHO

Unaweza kujiuliza ni watu gani wako kwenye hatari ya kuugua ugonjwa huu? Jibu ni kwamba ni wale wote ambao ukoo wao una kawaida ya kuwa na wagonjwa wa maradhi haya ya presha ya macho.

Wengine ni watu wanaougua ugonjwa wa kisukari, watu wenye umri zaidi ya miaka 40, watu walioumia macho, watu wanaotumia dawa fulanifulani kama predinisolone ambazo huweza kuathiri macho, watu waliopata ajali na kuumia macho na watu wasioona vizuri wanaweza kupatwa na presha ya macho.

 

DALILI ZA UGONJWA HUU

Zipo dalili nyingi za mtu mwenye presha ya macho na mara nyingi ugonjwa huu dalili zake haziji moja kwa moja kwani huja kwa kujificha sana bila muhusika kujua.

Mgonjwa anakuja kugunduliwa kwenye hatua mbaya kabisa ambayo ni ya hatari kwake. Moja ya dalili ya maradhi haya ni mtu kushindwa kuona mbali na pembeni, mgonjwa kuwa na macho mekundu na kusikia maumivu makali ya macho.

Dalili nyingine ni mgonjwa kuhisi kichefuchefu na kutapika, kuona kama mawingumawingu au ukungu.

 

VIPIMO VYA PRESHA YA MACHO

Ili kugundua kwamba una tatizo la presha ya macho unatakiwa uonapo dalili huzo kwenda haraka hospitali kumuona daktari ambaye atatumia vipimo maalumu kupima presha yako ya macho.

Baada ya hapo atapima kuangalia kama mishipa ya fahamu inayohusika na kuona imeathirika kiasi gani. Mara nyingi kipimo cha tenometry ndicho hutumika kupima presha ya macho.

 

TIBA YA MARADHI HAYA

Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu kabisa lakini kuna dawa za kutumia kwa muda wote wa maisha yako ambazo zitakua zinapunguza presha ya macho yako.

Dawa hizo ni zile za matoni kama vile timolol lakini pia wakati mwingine kuna aina za upasuaji hufanyika kuweka matundu kwenye iris ili kuachia majimaji yanayoleta tatizo kupita na kupunguza presha ya macho.

Mtu anaweza kujiuliza je, unaweza kuzuia ugonjwa huu, jibu ni kwamba huwezi kuzuia maradhi haya lakini unaweza kuzuia upofu kwa kuanza matibabu mapema na kuyafuatilia matibabu kwa umakini kama utakavyoelekezwa na daktari wa macho.

USHAURI

Uonapo dalili tulizotaja hapa, wahi kumuona daktari ili kuepusha upofu.

Maoni / Ushauri | 0713 777983

Comments are closed.