The House of Favourite Newspapers

Dar Nyekundu, Kariakoo Yasimama Mapokezi Ya Simba (Picha + Video)

 

HATA kama kuna mtu alikuwa hajui nguvu ya Simba, jana Jumatano alisikia kishindo chao walipotua Dar es Salaam. Hata kama hakusikia alihadithiwa na rafi ki au kuona kwenye mitandao ya kijamii.

 

Ilikuwa si mchezo. Kuanzia majira ya saa 6 mchana kishindo na nderemo za Simba zilianza kusikia mitaa ya Kibaha mkoani Pwani yalipoanzia maandamano makubwa ya mashabiki na wanachama huku wachezaji wakipanda gari la wazi wakionyesha kombe walilotwaa msimu huu.

 

Ingawa walipofi ka maeneo ya Luguruni gari la wazi lililokuwa limebeba Wachezaji na Kombe liliharibika, walilazimika kushuka fasta na kupanda jingine ambalo awali
liliandaliwa spesho kwa mashabiki.

Shangwe likaendelea. Msafara huo wa Simba uliteka sehemu kubwa ya Barabara ya Morogoro kuja Dar es Salaam ambapo watu wa kada mbalimbali waliacha kazi zao na kujazana kwa mamia barabarani huku wakishangilia mdogomdogo mpaka kwenye makao makuu ya klabu hiyo iliyopo Msimbazi.

Hatahivyo, nyomi ambalo Simba walilikuta kwenye mitaa mbalimbali lilikuwa chamtoto ya lile la Msimbazi. Hapo ilikuwa ni komesha kwani mitaa mbalimbali na maduka yalilazimika kusimamisha biashara kwa muda kutokana na msongamano mkubwa wa watu ambao hawakuwahi kuushuhudia kabla.

Hata usafi ri ukiwemo wa daladala na mwendokasi mitaa ya Kariakoo ulisimama kwa muda kwa vile hakukuwa na njia ya kupenya. Nyomi lilikuwa si mchezo. Wengi waliojitokeza walikuwa wametupia uzi wenye rangi nyeupe na nyekundu zilizofanya maeneo mbalimbali kuwa kwenye muonekano wa kipekee wa kupokea mabingwa.

 

Walipotua Msimbazi pale Klabuni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ni nahodha msaidizi wa Simba, akamkabidhi Kombe Paul Makonda ambae ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyekuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo. Kocha wa Simba nae alishuka na kushangilia na Makonda pamoja na mashabiki na wanachama wengine ambapo walikaa hapo kwa dakika kadhaa msafara ukaelekea hotelini maeneo ya Mbezi Beach.

Katika msafara huo, Tshabalala ndiye aliyekuwa akiwaimbisha mashabiki kuimba; “Mwakani.. tunachukua tena.” Jioni ya jana wanachama maarufu wa Simba na Wachezaji walikula Bata la kufa mtu kwenye hoteli ya Seascape Mbezi Beach ambako ndiko wanakoweka kambi.

 

Safari nzima ya Simba ilianza Kibaha majira ya mchana ambapo ilitumia zaidi Barabara ya Morogoro, ikikatisha maeneo ya Kibamba, Mbezi, Kimara na Ubungo ambapo mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakiacha biashara zao na kuja kushangilia kwa muda na wachezaji wao.

Maeneo ya Kibamba na Mbezi wauza bidhaa ndogondogo za vyakula waliacha maeneo yao na kukimbilia uwanjani kwa ajili ya kushangilia ubingwa wao huo huku eneo la Ubungo ambapo kunafanyiwa ukarabati wa barabara, watengenezaji (wakandarasi) walikatisha shughuli hiyo na kujiunga na mashabiki wenzao kwa ajili ya kushangilia msafara huo.

Stori na SAID ALLY, Dar es Salaam | Picha na Richard Bukos – GPL

Comments are closed.