The House of Favourite Newspapers

Daraja la Simiyu Mwanza-Musoma Lafungwa

0

DARAJA la Mto Simiyu lililoko wilayani Magu katika barabara kuu ya Mwanza-Musoma limeharibika, hivyo serikali kulifunga kwa siku kumi ili kupisha matengenezo makubwa. Daraja hilo limeharibika kutokana na uchakavu uliosababisha vyuma kukatika.

 

Akiwasilisha taarifa ya ufungwaji wa daraja hilo Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Marwa Rubirya, alisema ameifunga barabara hiyo kuanzia jana hadi Machi 8, mwaka huu ili kupisha matengenezo makubwa ya daraja hilo.

 

Mhandisi Rubirya aliongeza kuwa wameamua kufanya matengenezo ya haraka ili kujiepusha na athari zitakazoweza kujitokeza kwa sababu kuchelewa kwa ujenzi huo unaweza kuwasababishia athari watumiaji wa barabara hiyo.

 

Alisema kuwa barabara hiyo imefungwa ili kupisha matengenezo kuanzia saa tatu usiku hadi saa 11 asubuhi, huku akiomba ushirikiano wa polisi katika kutekeleza kazi hiyo.

 

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa daraja hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema kutokana na changamoto hiyo njia zitafungwa kwa muda uliopangwa kwa siku kumi ili kupisha matengenezo hayo.

 

Alisema serikali ina mpango wa kujenga daraja jipya, hivyo hatua zinazofanyika sasa ni za muda mfupi, na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu ili waboreshewe njia itakayowanufaisha na kuendeleza ujenzi wa taifa.

Leave A Reply