The House of Favourite Newspapers

DC Chongolo Azindua Maonyesho Bidhaa za Ngozi

0
Mwandishi wa mtandao huu,  Neema Adrian (kulia),  akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wauzaji wa bidhaa hizo za ngozi katika maonyesho yanayofanyika katika viwanja wa Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo,  amesema kuwa katika kutatua changamoto ya kupata soko la uhakika la bidhaa za ngozi, wilaya hiyo imejipanga kuwatafutia maeneo wazalishaji wa ndani ambapo wote watakaa sehemu moja kwa ajili ya uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hizo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, akitazama kiatu cha ngozi kwenye maonyesho hayo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa za ngozi yanayofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers,  amesema kuwa mkakati huo utasaidia kuinua uhakika wa soko kwa wazalishaji.

 

Amefafanua kuwa maonesho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza katika wilaya hiyo na kwamba ni lazima kila mwananchi ajenge utamaduni wa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuwataka kuondokana na dhana ya kuona bidhaa zinazotoka nje ndiyo bora zaidi.

 

…Akiangalia mkanda wa ngozi.

“Ukienda kwenye nchi za wenzetu hasa zilizoendelea, wao wanathamini kwanza cha kwao, cha mwingine baadaye, na sisi tukifikia hatua hiyo tutafanikiwa sana, lakini tutafikaje hapo ni lazima kuanzia sasa tuamke tuanze kupenda vya kwetu,” amesema.

 

Ameongeza kuwa uwepo wa maonyesho hayo utaongeza tija na mipango madhubuti ya kuhakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu sambamba na kuongeza wigo mpana wa kutangaza bidhaa hizo na wananchi kupenda kuzitumia.


“Uwepo wenu hapa utawezesha wale wananchi ambao wanakuja kununua bidhaa zenu, ndiyo watakuwa mawakala kwa wananchi wengine ambapo na wao watapenda kuja kununua bidhaa hizi bora na nzuri za Tanzania,” amesisitiza. 

 

Naye Diwani wa Kata ya Kawe,  Muta Rwakatare,  amempongeza Chongolo kwa kubuni na kufanikisha kuwepo kwa maonyesho hayo.

Amesema kuwa kutokana na umahiri aliokuwa nao mkuu huyo wa wilaya wa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, anaamini kuwa sasa ni wakati wa wajasiriamali hao kunufaika kwani changamoto zao pia zimefikia kikomo.

 

Pia amempongeza Rais  John Magufuli kwa kuwa mstari wa mbele katika kusisitiza uchumi wa viwanda na kwamba hadi sasa tayari nia hiyo imefanikiwa kwa asilimia kubwa.

 

Kiti cha ngozi ni baadhi ya bidhaa za ngozi zinazoonyeshwa.

Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Patricia Henjewele, amesema kuwa wazo la kuwepo kwa maonyesho hayo lilitolewa na  Chongolo wakati wa maonyesho ya Nanenane ambapo alielekeza kuandaliwa kwa mpango-kazi wa kuwa na maonyesho hayo.

Chongolo akizungumza kwenye maonyesho hayo.

Amesema kuwa kabla ya kufanyika kwa maonyesho hayo, awali yalifanyika mafunzo ya siku nne ambayo yalienda sambamba na maonyesho ya bidhaa hizo kwa siku moja yaliyofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

 

Henjewele amesema kuwa maonyesho hayo ya siku nne yatafikia kilele Desemba 15, mwaka huu, ambapo bidhaa zote za ngozi vikiwemo viatu, mikoba, mikanda na mabegi ya shule ya wanafunzi yanapatikana hapo.

 

HABARI:NEEMA ADRIAN
PICHA: RICHARD BUKOS GPL

Leave A Reply