The House of Favourite Newspapers

DC Muro Apokea Pikipiki Kutoka CRDB, Azikabidhi Polisi

Benki ya CRDB imekabithi msaada wa pikipiki tano zenye thamani ya shs 10 milioni kwa kituo cha polisi USA River kwa ajili ya kuimarisha doria na usalama wa wananchi na mali zao.

 

Akizungumza wakati wa kukabithi msaada huo katika kituo cha polisi USA River, Mkurugenzi wa wateja wadogo na wa Kati katika benki hiyo, Boma Raballa alisema kuwa, benki hiyo inatambua na kuthamini sana umuhimu wa usalama wa raia na mali zao na hivyo wamekuwa wakishirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Raballa alisema kuwa, utoaji wa msaada huo ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango mkakati wa benki hiyo wa kusaidia huduma za kijamii kupitia sera ya kusaidia jamii, na kwa kufanya hivyo jeshi hilo litaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zake kwa kufanya doria katika maeneo mbalimbali.

 

“Benki ya CRDB kwa kutambua umuhimu wa jeshi hilo ikiwa sehemu ya jamii na mdau mkubwa wa maendeleo imekuwa ikichangia katika kuboresha utendaji wa jeshi la polisi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi Marangu Kilimanjaro, pamoja na ununuzi wa gari kwa ajili ya kituo hicho na maeneo mengine mbalimbali hapa nchini “alisema Raballa.

 

 

Naye Meneja wa kanda ya kaskazini wa benki hiyo, Chiku Issa alisema kuwa, watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano na jeshi hilo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

 

Chiku alisema kuwa, wamefikia hatua ya kusaidia usafiri huo kutokana na changamoto ya usafiri inayowakabili ,jambo ambalo limekuwa likipunguza ufanisi wa utendaji kazi kwa askari hao na hivyo pikipiki hizo zitasaidia sana kuongeza ufanisi kazi kwa wakati katika jeshi hilo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, aliishukuru benki hiyo kwa msaada mkubwa wa usafiri huo wa pikipiki kwa askari wake ambao sasa umewezesha kuzinduliwa rasmi kwa zoezi la kwanza la doria ya pikipiki katika wilaya hiyo.

 

Muro alisema kuwa, msaada wa pikipiki hizo utasaidia sana kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi katika wilaya hiyo kwa kufanya doria katika vichochoro mbalimbali ambavyo vilikuwa havifikiki kwa haraka pamoja na kusimamia usalama barabarani.

Aidha Muro aliwataka askari polisi kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyowekwa badala ya kuzitumia kwa maslahi yao binafsi, huku wakihakikisha ulinzi unaimarishwa katika maeneo mbalimbali kwa kutumia vitendea kazi hivyo.

Comments are closed.