The House of Favourite Newspapers

Dhamana ya Aveva, Kaburu Ngoma Bado Mbichi!

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi juu ya dhamana ambayo walifutiwa waliokuwa viongozi wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Godfrey Nyange (Kaburu), wiki iliyopita.

 

Hiyo ni baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kushindwa kutoa maamuzi hayo kutokana na muda wake kuwa mfupi ambao angeutumia kupitia hoja zilizotolewa na pande mbili za mashtaka na utetezi.

 

Hakimu huyo alitakiwa kutoa maamuzi kwa mara nyingine kuhusiana na kuwafutia mashitaka ya utakatishaji fedha washitakiwa wawili Evans Aveva na Godfrey Nyange ambayo yaliwapa nafasi ya kupata dhamana.

Hata hivyo, maamuzi hayo ya awali ya Hakimu Simba yalipingwa na upande wa jamhuri ambapo walikata rufaa Mahakama Kuu kuomba maamuzi yote yaliyotolewa yaweze kutenguliwa.

 

Simba ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11, mwaka huu, ambapo atatoa uamuzi juu ya kesi hiyo. Wiki iliyopita mahakama ilitoa uamuzi na kuwafutia mashitaka mawili ya utakatishaji fedha waliokuwa viongozi wa Simba lakini baadaye upande wa jamhuri ulikata rufaa juu ya maamuzi hayo.

 

Aveva na Kaburu wanashitakiwa kwa makosa tisa ambapo mawili yakiwa ni ya utakatishaji fedha na mengine ya kughushi ambapo katika kesi hiyo waliunganishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Simba Zacharia Hans Poppe.

Comments are closed.