The House of Favourite Newspapers

DIAMOND AMWAGA MAMILIONI KWA VIJANA, WALEMAVU NA WANAWAKE TANDALE

Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

KUFUATIA kusherehekea siku yake ya kuzaliwa eneo alilokulia la Tandale- Maguniani jijini Dar na kukabidhi bima ya afya kwa watu 1,000, bodaboda 20 kwa vijana pamoja na kina mama 100 kupatiwa mitaji ya shilingi laki moja kila mmoja,  staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameandika historia, Risasi Jumamosi linaripoti.

Diamond ambaye amezaliwa Oktoba 2, 1989, jana aliamua kushereheka siku yake hiyo ya kuzaliwa kwa kushiriki kutoa misaada katika eneo hilo akiambatana na wasanii na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika Uwanja wa Maguniani.

NI HISTORIA

Mbali na kutoa vitu hivyo vingi vya thamani kama msanii wa kwanza nchini, tukio hilo liliandika historia pia kwa kujaza uwanja huo wa mpira kiasi cha watu kupanda hadi kwenye paa za nyumba ili waweze kushuhudia kilichokuwa kikiendelea.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Geofrey Mngereza akisalimiana na Diamond Platnumz.

WCB WAFUNGUA PAZIA

Katika hafla hiyo, mshereheshaji (MC), Babu Tale alimuita jukwaani Mbwana Yusuf ‘Mbosso’ na kutoa kionjo cha wimbo wake wa Hodari na baadaye alihitimisha kwa Wimbo wa Nadekezwa kabla ya kumpisha Lava Lava ambaye naye alijitambulisha.

 

BASATA NDANI B

aada ya kumaliza wasanii wa WCB, aliingia Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Geofrey Mngereza ambaye aliamsha shangwe kwa kuanza kurap jambo ambalo hakuwahi kulifanya tangu amekuwa kiongozi Basata.

“Niseme neno moja, mara nyingi watu wanapofikia mfanikio wanasahau walipotoka hasa wale waliotokea familia za wakulima, lakini nipende kutoa shukrani kwa Diamond kurudi alipotokea na kuleta fadhila kwa vijana wenzake. Mcheza kwao hutunzwa!”

 

SHIGONGO ATOA FUNDISHO

MC Babu Tale kabla ya kumtambulisha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Group, Eric Shigongo alianza kwa kumuelezea kifupi namna alivyoanzisha safari ya muziki wa Diamond. “Shigongo amekuwa mtu kwa kwanza kumlipa Diamond pesa nyingi, amekuwa akimpa sapoti kubwa kwa kumuandika lakini ni masikini mwenzetu na vyote hivyo viliwezekana hadi leo tukatusua,” alisema Babu Tale na kumpatia kipaza sauti Shigongo.

 

“Nyumbani oyee! Naishi jirani tu hapo na nyinyi, asiwepo mtu yeyote wa kuwadharau kwa sababu mnatoka Tandale, niwashukuru wote kwa uwepo wenu na najisikia vizuri kuwa mbele yenu. “Miaka michache iliyopita nilikuwa hapa Tandale na nyinyi na nikawaambia kila kitu kinawezekana kufanikiwa katika maisha haijalishi umetoka familia gani…,” alisema

Shigongo na kuongeza: “Nyie mliopo hapa ndiyo mtanunua nyumba zote zilizopo Masaki (jijini Dar) kwani zinawasubiri, wengine kesho na kesho kutwa mtakuwa marais wa nchi hii. Jiepusheni na tabia mbaya, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya. “Inawezekana mkawa mabilionea, chukua hatua leo muiletee familia na nchi heshima namuomba Mungu wote mliokuwa mbele hapa muweze kufanikiwa,” alimaliza Shigongo.



MEYA KUMPA DIAMOND MTAA

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta aliamsha shangwe kwa umati uliofurika baada ya kutamka kumpatia Diamond mtaa. “Mimi kama Meya wa Kinondoni najivunia sana na bado nafikiria ni mtaa gani tumpe jina bado tunachanganyikiwa, basi mpaka tunapofunga hafla hii Diamond atakuwa amechagua mtaa au shule, lazima tuoneshe tunamthamini nabii huyu kwa kuthamini jamii yao,” alisema Meya Benjamini.

JACQUELINE MENGI AIBUA SHANGWE

Mjasiriamali Jacqueline Mengi aliibua shangwe baada ya kuingia jukwaani ambapo mashabiki wengi walisikika wakimtaka kwanza avue miwani jambo alilolitekeleza. “Nataka niwape ushauri wakina mama wenzangu na kina kaka, hakuna kitu kama kuwa na malengo, mtapewa zawadi au miradi, pesa ya biashara ni kwenye biashara nawategemea wakina mama mkipata mtaji kesho tukirudi tuje kuwakuta ni wafanyabiashara wakubwa na vijana nyie ndiyo nguvu kazi ya taifa inabidi mjiamini kama mnaweza kama ilivyo kwa Diamond.”



HAJI MANARA AGEUKA KIVUTIO

Katika hatua nyingine, msemaji wa Timu ya Simba, Haji Manara aligeuka kivutio baada ya kuonesha mbwembwe za kucheza nyimbo za Simba huku mara nyingi akiisifia timu hiyo. “Nimekuja na mipira na nataka kila shule za Tandale kuwa na mipira minne pamoja na jezi hizi za Simba,” alisema Manara na kumkabidhi Diamond mpira pamoja na jezi.

MAKONDA AMTAKA DIAMOND AOE

Shangwe nyingine ilikuwa kwa Makonda baada ya kupewa nafasi na kueleza jinsi alivyokuwa mlezi wa WCB na kumtaka Diamond aoe kabla mwaka haujaisha. “Leo hii Diamond akimtaka hata mwanamke wa aina gani atampata kwa sababu ana kipaji. Kuna mstahiki Meya hapa (Benjamini Sitta) nimemwambia mwaka huu ukiisha asipooa namfunga, kuna mwingine naye anaitwa Majizzo yeye juzi kaniwahi kamvisha pete Lulu (Elizabeth Michael). “Lakini nilikuwa najiuliza huyu naye (Diamond) tumtie ndani au tufanyeje? Lakini nimegundua kwa kazi aliyonayo, Diamond nampa miaka acha kwanza aendelee kuwa sukari ya mioyo ya watu, namtaka baadaye awe zaidi ya kina 50 Cent na Jay Z si mnaona hata Jay Z alifanya muziki akaweka mambo yake.

Comments are closed.